In Summary

Watumiaji wengi wa mtandao wa Twitter wameliona tukio la kutekwa kwa MO kama mwendelezo wa matukio mengine kadhaa ya utekaji yaliyowahi kutokea huko nyuma.


Dar es Salaam. Watumiaji wa mtandao wa Twitter nchini wameelezea hasira zao kwa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara mashuhuri Mohammed Dewji maarufu Mo huku wakisema ni mwendelezo wa matukio hayo nchini.

MO, ambaye anatajwa kuwa bilionea wa namba moja kijana barani Afrika, alitekwa asubuhi ya leo Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colosseum, Dar es Salaam alipokuwa amekwenda kwa ajili ya kufanya mazoezi na hadi mchana, mwanahisa huyo mkuu wa klabu ya mpira wa miguu ya Simba, hakuwa amepatikana huku Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakisema wameanza uchunguzi na tayari wanawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo.

Katika maoni yao, Watanzania walioko Twitter (#TOT), kama wanavyojiita wenyewe, wameelezea kushtushwa kwao na taarifa za MO kutekwa wakisema ni mwendelezo wa yale ambayo tayari yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini. 

#TOT wametumia tukio la kutekwa kwa MO kuikumbusha Serikali na jamii kwa ujumla ya kwamba, tukio hilo ni sehemu tu ya tatizo kubwa la kiusalama ambalo linaikabili nchi.

Akiandika katika mtandao huo wa Twitter baada ya taarifa iliyotolewa na polisi kuwa inawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema matukio ya uhalifu yamekuwa yakitokea lakini hakuna hatua za haraka ambazo zimekuwa zikichukuliwa.

Fatma amerejea tukio la kuvamiwa kwa ofisi za IMMA Advocates mchana ambalo sasa limetimiza takriban mwaka.

Katika mchango wake, katibu mstaafu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSN), Alphonce Lusako, ameandika katika mtandao huo wa Twitter kwamba ongezeko la matukio ya utekaji na kupotea yanasababishwa na kile alichokiita “kansa ya watu kutokuchukuliwa hatua na unafiki.”

Tito Magoti ni mwanasheria kutoka katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ameandika kuwa Taifa linahitaji kuelezwa nini hasa kimemtokea MO na ni nani walioko nyuma ya vitendo hivyo vya kihuni. 

“Tuna ndugu zetu ambao wamekuwa wahanga (waathirika) wa matukio kama haya huko nyuma – ni muhimu tukaambiwa nini kinaendelea na hatua stahiki zikachukuliwa,” ameandika.

Watumiaji wengine katika mtandao huo wa kijamii wamejibu andiko la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), January Makamba ambaye alieleza kusikitishwa kwake na tukio hilo, kwa kumjia juu wakihoji kwa nini hakuonyesha kuguswa katika matukio mengine kama hayo.

Makamba ameandika katika mtandao wa Twitter akieleza kusikitishwa kwake na taarifa za kutekwa kwa MO ambaye amemwita “rafika yangu” akisema anaamini polisi watatoa taarifa kamili na kuwaomba wafuasi wake katika mtandao huo wa kijamii kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Mmoja wa watumiaji, @niyonzimazabron, akichangia katika andiko hilo la Makamba, alisema hakuwahi kumuona waziri huyo akihuzunishwa wakati taarifa za kupotea kwa Ben Saanane (msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), Azzory Gwanda (mwandishi wa Gazeti la Mwananchi) na wengineo wengi zilipoibuka. 

“Hivi tunaweza kuacha huu unafiki?” alihoji. Hata hivyo, Mwananchi linafahamu kuwa Makamba amekuwa na mwitikio huohuo aliokuwa nao kuhusu kutekwa kwa MO wakati taarifa kama hizo zilipokuwa zinajitokeza akitumia mtandao huohuo wa Twitter kulaani na kukemea vitendo hivyo.

Wakati wengine wakilaumu na kunyooshea wengine vidole, baadhi wamekuwa wakihimiza subira huku wakitaka uchunguzi ufanyike. Mmoja kati yao,@mwalimu053 21m21, ameandika: “MO ni mfanyabiashara mwenye shughuli nyingi za kibiashara. Hili jambo linapaswa kuangaliwa katika pande zote. Uchunguzi unaweza kubaini haya.”

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameandika katika mtandao huo akisema, ameshtushwa na habari za kutekwa kwa MO na kutoa wito kwa wafuasi wake katika mtandao huo kutoa taarifa ambazo zinaweza kusaida kupatikana kwa MO na kuwataka wamuweke MO na familia yake katika sala na maombi yao.

“Ni matumaini yetu ya kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitachukua hatua stahiki,” ameongeza kiongozi huyo wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Pia, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ni miongoni mwa wanasiasa na watu mashuhuri kadhaa walioonyesha kuguswa na tukio hilo na kutaka vyombo vya ulinzi na usalama kuharakisha uchunguzi.