In Summary

Kutokana na kujitoa kwa wasichana hao, uwezekano wa Burundi kupata mwakilishi katika mashindano ya urembo ya dunia sasa uko shakani.


Shindano la urembo la Miss Burundi limeingia dosari baada ya washiriki 16 kujiondoa, wakidai kuna ubabaishaji wa zawadi za washindi, hasa fedha taslimu.

Wasichana hao 16 kati ya 17 waliosalia wamejiondoa wakati shindano hilo likiwa limefikia hatua ya fainali na hivyo kuweka uwezekano wa nchi hiyo kutopata mwakilishi katika mashindano ya dunia.

Hatua hiyo sasa inaonekana kutishia uwezekano wa kufanyika shindano hilo kwa mwaka huu 2018.

Kupitia waraka ulioandikwa na wasichana hao wameeleza sababu ya kujiondoa ni baada ya kugundua udanganyifu kwenye zawadi atakayotunukiwa mshindi wa kwanza na wa pili.

Wasichana hao wamehoji uaminifu na heshima ya waandaaji wa shindano hilo ambao ni Burundi Events na wanataka kuhakikishiwa zawadi zao.

Akizungumzia tatizo hilo mmoja wa waandaaji alisema haiwezekani kuendelea na shindano hilo bila ya kuwa na washiriki.

Mdhamini wa Burundi Events, Amine El Kosseifi aliuambiwa mtandao wa burundi.eu kuwa atazungumzia suala hilo baadaye. Kwa upande wake, Wizara ya Utamaduni na Michezo ambayo iliahidi kuwa ingeisaidia Burundi Events kifedha, bado haijazungumzia kujiondoa kwa washiriki hao.

Katika akaunti ya Twitter, ofisi wa Ofisi ya Rais anayehusika na masuala ya habari na mawasiliano, Willy Nyamitwe alitaka kampuni hiyo ichukue hatua.

"Inasikitisha. Burundi Events inatakiwa itafute suluhisho la udhaifu huo ambao unasababisha fedheha kwa taifa la Burundi. Shindano la Miss Burundi si la mtu mmoja, bali la taifa," ameandika Nyamitwe.

Imeelezwa kuwa hapo awali waandaaji wa shindano hilo walisema mshindi angejinyakulia gari jipya pamoja na kiwanja chenye ukubwa wa mita mia nne ikiambatana na tuzo pamoja na pesa, suala ambalo wasichana hao wamedai hakuna uhakika wa zawadi kuwepo hadi sasa kwa ajili ya washindi.

Kampuni ya Burundi Events inayoandaa Miss Burundi imeahirisha fainali hiyo iliyopangwa kufanyika Julai 21, 2018 na sasa itafanyika Julai 28.