In Summary

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza sera na  mipango madhubuti  ya kuboresha maisha na kupunguza hali ya  umasikini nchini.

Dodoma.  Waziri wa Fedha na Mipango, Phillip Mpango amesema, kiwango cha idadi ya watoto kimepungua kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49.

Akizungumza bungeni leo Juni 14 wakati akiwasilisha mwenendo wa hali ya uchumi kwa 2017, amesema mwaka 2013, wastani  wa uzazi kwa wanawake wa umri huo ilikuwa watoto 5.3 lakini sasa imepungua na kufikia watoto 5.1 kwa mwaka 2017.

Kadhalika Dk Mpango amesema umri wa kuishi umeongezeka kutoka wastani wa miaka 62.2, 2013 hadi 64.4 mwaka 2017.

Katika hotuba hiyo inabainishwa kuwa matarajio  ya Serikali ni kuendelea kuboresha huduma za jamii ili ifikapo 2020 kila  Mtanzania aweze kuishi kwa wastani wa miaka 66.1.

“  Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 42.8 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2013 hadi kufikia watoto 34.5 mwaka 2017 na matarajio ni kuendelea kupungua hadi kufikia 32.6 mwaka 2018,” anasema Dk Mipango.  

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza sera na  mipango madhubuti  ya kuboresha maisha na kupunguza hali ya  umasikini nchini.