Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa sasa inaundwa na nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Huu ni umoja wa kikanda wenye malengo ya kiuchumi, kijamii, kiusalama, kisiasa hata kiutamaduni.

Umoja huu umepitia hatua kadhaa kutoka umoja wa forodha hadi soko la pamoja. Kuelekea umoja wa kina zaidi, nchi wanachama zinajipanga kuingia katika umoja wa fedha au sarafu utakaofuatiwa na shirikisho la kisiasa.

Mapema mwezi huu, walipokutana Arusha kwenye mkutano wao, wakuu wa nchi zinazounda jumuiya hii waliridhia kuanza kwa safari ya kuelekea katika umoja wa sarafu. Umoja wa sarafu ni jambo muhimu linalopaswa kueleweka kwa wengi.

Umoja wa sarafu au fedha unakuwapo pale nchi huru mbili au zaidi zinapokuwa na sarafu moja. Kwa Afrika mashariki kwa mfano, sarafu hii inaweza kuwa Shilingi ya Afrika Mashariki.

Nchi hizi huweza kuwa na safari tofauti lakini zikawa na kiwango cha kubadilishana sarafu kilicho sawa. Kiwango hiki ni lazima kisimamiwe na kufuatiliwa na benki kuu moja au benki kuu za nchi husika.

Katika hali hii nchi huwa na sera za fedha zinazoratibiwa kwa karibu ili zifanane kwa kiwango kikubwa miongoni mwa wanachama. Umoja wa sarafu huambatana na soko la pamoja, riba na viwango vya kodi vinavyolandana.

Umoja huu si mgeni duniani. Umoja wa Ulaya, kwa mfano, licha ya kila Taifa kuwa na sarafu yake lakini zinayo ya pamoja, zinatumia sarafu ya Euro. Mfano mwingine ni umoja wa sarafu wa Afrika magharibi.

Faida na changamoto

Umoja wa sarafu ni mzuri kwani huchangia kuhamasisha kuleta muungano wa karibu zaidi kwa nchi wanachama. Unafanya maisha ya kiuchumi ya biashara na uwekezaji kwa wanachama kuwa rahisi, yenye ufanisi na ustawi zaidi.

Hurahisisha matembezi wa watu, wafanyakazi na mitaji ndani ya jumuiya, huondoa hasara za kuwa na sarafu tofauti zinazohitaji kubadilishwa ili kufanikisha biashara kati ya mataifa wanachama.

Umoja wa sarafu unaweza kugubikwa na changamoto kadha wa kadha. Taifa zinaweza kupenda kuwa na sera za uchumi mpana ili kukidhi mahitaji ya nchi husika.

Katika umoja wa sarafu ni lazima nchi ziwe pamoja katika sera za msingi. Ikitokea mtikisko wa fedha na uchumi kwa mfano, nchi moja haitaweza kutumia sera za fedha inazotaka ili kujinasua katika mtikisiko kama nyingine hazijakubali.

Kwa mfano nchi haiwezi kurekebisha viwango vya kubadili fedha ili kufanikisha malengo ya kibiashara hata ya kisekta kama vile viwanda. Haya yalionekana Ugiriki, Ireland na Ureno katika mtikisiko wa fedha wa ukanda wa Euro uliotokea mwaka 2010.

Vigezo na masharti

Kusudi umoja wa sarafu uwe madhubuti ni lazima vigezo na masharti kadhaa yazingatiwe na nchi wanachama. Baadhi ya vigezo na masharti haya ni nchi wanachama kuwa na mambo ya msingi ya uchumi mpana yanayoelekea kufanana.

Mambo haya ni pamoja na mfumoko wa bei, nakisi ya bajeti, deni la Taifa, riba, kiwango cha kubadili fedha na, sera za fedha na kodi zinazoendana.

Nchi hukubaliana viwango, vigezo na masharti ikiwamo tarehe ya kuvifikia. Kati ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa hili ni uwezekano wa nchi zote kutimiza vigezo na masharti yote kwa wakati mmoja.

Kama ilivyo vya hatua nyingine za muungano wa kikanda wa nchi, umoja wa sarafu nao ni mchakato sio tukio. Ni sawa na kujenga Jiji la Roma, haiwezekani na haitowezekana kukamilika kwa siku moja.

Kukamilisha hili pia haitakiwi kukurupuka na kuharakisha bila umakini wa hali ya juu. Ubora na umadhubuti wa umoja wa sarafu ni msingi imara wa umoja utakaodumu na kufanikisha malengo yanayotarajiwa.

Ni muhimu kuyaacha mambo yaliyomo kwenye mchakato wa kuunda umoja wa sarafu yafuate mkondo wake. Hata hivyo sio vibaya kuwa na vichocheo vya kuisukuma safari hii.

Ushauri

Kati ya mambo ya msingi na muhimu zaidi kufanywa ili umoja wa sarafu ufikiwe na kufanikiwa, kuna haja kubwa ya kutoa elimu. Hii iwe ni elimu kwa watu wote si wa kawaida peke yao.

Mahitaji ya elimu ni makubwa hasa kwa watu wa kawaida. Pamoja na mambo mengine, elimu itapaswa kujikita katika kujua na kutafsiri umoja wa sarafu na maana yake katika maisha ya kila siku ya mtu wa kawaida wa Afrika mashariki na kwingineko.