In Summary

Washukiwa hao wengine walikuwa wameajiriwa kama wafanyakazi wa kufagia na kusafisha nyumba wakati wa kutekelezwa kwa wizi huo siku moja kati ya Desemba Mosi na mapema Januari

Harare, Zimbabwe. Watu watatu wamefikishwa mahakamani nchini Zimbabwe wakishtakiwa kuiba mkoba uliokuwa na Dola 150,000 za Marekani, mali ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe.

Watuhumiwa hao wa wizi wanadaiwa kutumia fedha hizo kununua magari, nyumba na mifugo ikiwemo nguruwe na ng’ombe.

Ndugu wa rais huyo wa zamani, Constantia Mugabe ni miongoni mwa walioshtakiwa, kwa mujibu wa taarifa katika vyombo vya habari vya Serikali.

Mwanamke huyo anadaiwa kuwa na funguo za nyumba ya kijijini kwa Mugabe iliyopo eneo la Zvimba karibu na mji mkuu wa Harare na ndiye aliyewasaidia wengine kuingia na kufika ulikokuwa mkoba huo.

"Johanne Mapurisa alinunua gari aina ya Toyota Camry na nyumba ya Dola 20,000 baada ya kisa hicho," amesema mwendesha mashtaka wa Serikali, Teveraishe Zinyemba akiiambia Mhakama ya Chinhoyi.

"Saymore Nhetekwa alinunua gari aina ya Honda na mifugo migine ikiwemo nguruwe na ng'ombe wa thamani ambayo haijulikani.

Mugabe, ambaye kwa sasa ana miaka 94 aliondolewa madarakani na jeshi la Zimbabwe mwaka 2017.

Tangu alipoondolewa, Mugabe amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kutembea na alikaa miezi kadhaa nchini Singapore akipokea matibabu.