In Summary

Serikali imesisitiza kwamba deni la Taifa ni dola za Kimarekani 8.7 bilioni (sawa na kwacha 82,804 bilioni au Sh19,707 trilioni)

Masoko ya fedha ya kimataifa na wahisani wamezidi kuwa na wasiwasi juu ya “madeni yaliyofichika” nchini, hali inayofanana na kilichoitumbukiza katika mgogoro mkubwa wa kifedha nchi jirani ya Msumbiji.
Kwa wiki kadhaa wahisani wamekuwa wakihitaji majibu kuhusu kiwango halisi cha ukopaji fedha nchi za nje, lakini maofisa wamepuuza madai ya kuwepo madeni yaliyofichwa.
Serikali imesisitiza kwamba deni la taifa ni dola za Kimarekani 8.7 bilioni (sawa na kwacha 82,804 bilioni au Sh19,707
trilioni), lakini kumekuwa na wasiwasi kwamba deni linaweza kuwa mara mbili ya hilo.
Madai hayo yaliibuliwa na baadhi ya wawekezaji wa Zambia na wa kigeni ambao bado kilichoikuta Msumbiji kuhusu mgogoro wa madeni kipo mioyoni mwao.
Mwaka 2016, wahisani wa kimataifa walisitisha msaada wa fedha kwa Msumbiji baada ya kuibuka kwamba nchi ilichukua mkopo wa Dola 2 bilioni za Marekani “bila kurekodi popote” kwa ajili ya kugharimia vyombo vya majini na vifaa vya kijeshi.
Hatua hiyo iliitumbukiza nchi maskini ya Msumbiji katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kifedha.
Serikali ya Msumbiji, tangu wakati huo iliacha kuwalipa wakopeshaji na inatafuta njia za majadiliano kuhusu mzigo wa deni lililopo.
Hivi karibuni shirika la fedha la Nomura la Japan lilihoji ukubwa wa deni la umma la Zambia huku ikidokeza kwamba Serikali inaficha kiasi cha deni la nje la muda mfupi.
Katika taarifa yake wiki iliyopita, mkurugenzi wa ushauri wa mikopo hatarishi wa shirika la EXX Africa alionya kuwepo kwa “ushahidi wa mikopo ambayo haijawekwa wazi” na kwamba Zambia imekosea kupiga hesabu ya deni jumuifu.