In Summary
  • Kesi ya kumiliki mali isiyolingana na kipato chake halali inayomkabili Ofisa Msaidizi wa Forodha wa TRA, Jennifer Mushi, haikuendelea kutokana na wakili kutokuwapo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na kesi inayomkabili Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi kutokana na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokuwapo.

Jennifer anakabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo la kukutwa akimiliki magari 19, mali isiyolingana na kipato chake halali.

Wakili wa Serikali, Daisy Makakala amedai leo Jumatatu Aprili 15, 2019 mbele ya  Hakimu Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuendelea, lakini wakili wa Takukuru hayupo.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kuendelea kwa leo hatuna shahidi lakini pia wakili husika kutoka Takukuru hayupo hivyo tunaomba tarehe nyingine,” alieleza Makakala.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 8, 2019 itakapoendelea kusikilizwa.

Magari anayodaiwa kumiliki yalitajwa kuwa Toyota RAV4, Toyota RAV4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota Wish na  Toyota Mark X.

Mengine ni Toyota Regiusage, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown,  Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry yote yakiwa na thamani ya Sh197,6 milioni mali ambayo hailingani na kipato chake halali.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo kati ya Machi 21, 2012 na  Machi 30, 2016 Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA kama ofisa forodha msaidizi alikutwa akiishi maisha ya kifahari yenye thamani ya Sh333.25 milioni fedha ambayo hailingani na kipato chake halali.