In Summary

Kwa kuwa kila mjasiriamali hulenga kutengeneza faida kutokana na biashara anayoifanya, mkurugenzi mtendaji wa hoteli ya kitalii ya Hyatt Regency, Garry Friend anashauri umuhimu wa kujitanu amaeneo mbalimbali ili kuongeza uhakika wa kupata faida.

Mabadiliko ya sera za Serikali hutoa fursa kwa wawekezaji na wajasiriamali wa sekta tofauti za uchumi kukuza biashara zao.

Akizungumza na gazeti hili kuelekea shindano la kampuni bora za kati (Top100) litakalofanyika Oktoba 25, mkurugenzi mtendaji wa Hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro, Garry Friend anasema Serikali kuhamishia makao makuu jijini Dodoma ni fursa nzuri ya kuwekeza endapo wajasiriamali wataiangalia kwa jicho makini.

“Mazingira ya biashara ni magumu, nadhani ni wakati sahihi sasa kwa wafanyabiashara kuangalia masoko mapya yanayokua kwa kasi kama Dodoma na Zanzibar ili kujiinua kibiashara,” anasema Friend.

Hoteli ya Hyatt Regency ni mdhamini mpya wa Top 100 yaliyoanza kufanyika tangu mwaka 2011 yakiratibiwa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu za fedha ya KPMG kwa kushirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Mkurugenzi huyo wa hoteli ya kisasa ya nyota tano inayopatikana jijii Dar es Salaam kampuni zinazolengwa kwenye shindano hilo ambazo ni zile zenye mauzo ya kati ya Sh1 bilioni na Sh20 bilioni kwa mwaka, zinapaswa kutumia fursa zinazojitokeza kila mara kuongeza mapato yao.

Katika mahojiano hayo, Friend anasema wafanyabiashara wamekuwa hawapanui masoko ya biashara zao jambo linalosababisha kasi ya maendeleo yao kuwa na mwendo wa kinyonga.

Kutokana na uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma kumekuwa na ugumu katika baadhi ya biashara hivyo ni vyema wafanyabiashara wakaangalia fursa zilizopo Dodoma na ikiwezekana wakafungua matawi huo.

“Niwashauri watu wanaotaka kuanzisha biashara kwenda Dodoma au Zanzibar ili kuona fursa zilizopo huko. Kuna fursa nyingi katika maeneo hayo niliyoyataja zikishikwa vizuri zinaweza kuleta matokeo makubwa,” anasema Friend.

Kuwekeza katika maeneo tofauti kimkakati, anasema ni jambo zuri katika biashara kwani eneo moja linapokuwa na mwenendo usioridhisha jingine linaleta ustahimilivu hivyo kuhakikisha kunakuwa na mapato ya kutosha wakati wote.

“Ukiwekeza maeneo tofauti uwekezaji wako unaweza kuleta faida kubwa kwa kuwa biashara inakuwa imepanuka hivyo kampuni ina nafasi kubwa ya kuendelea kukua,” anasema Friend.

Hata hivyo anasema ni muhimu kwa wafanyabiashara kufanya utafiti katika eneo husika kujua ni huduma au bidhaa gani inahitajika ili kuwa na tathimini ya uhakika wa faida mapema kabla ya kuwekeza.

Friend anasema analitazama shindano la Top 100 kama darasa linalofundisha uboreshaji wa huduma na bidhaa huku likiwa daraja kwa wafanyabiashara kupata masoko ndani na nje ya nchi.

Endapo washiriki watatumia vyema muungano unaoletwa na shindano hilo, anasema wanao uhakika wa kukuza shughuli zao kwa kupata mawasiliano ya wadau wengi wanaofanya shughuli tofauti tena kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Anasema mabadiliko yaliyopo zama hizi yanahitaji wasambazaji wenye bidhaa bora, na zile zinazotumia muda mrefu kuagizwa kutoka nje zinawalazimu wafanyabiashara husika kuwa na akiba ya kutosha kukidhi mahitaji ya wateja wao.

Lakini, kwa kutumia fursa hii inayowakutanisha wafanyabiashara wengi pamoja, inaweza kuwasaidia kukuza mtandao hata kujikuta wanapata wazo la kuboresha shughuli zao za kila siku.

Kiongozi huyo wa Hyatt anasisitiza zaidi ubunifu katika biashara kwani zikishamiri zitasaidia kutoa ajira kwa watu wengi zaidi.

Hyatt Regency ni miongoni mwaka hoteli za kifahari nchini ikiwa, ina jumla ya wafanyakazi 261 na inahudumia wateja wa ndani na kimataifa. Kushiriki kwake Top 100, Friend anaamini kutaisaidia hoteli hiyo kukua zaidi na kuongeza mvuto wake kwa washiriki.

Anasema kampuni ikishiriki Top100 inajiweka katika nafasi nzuri ya kudhihirisha uzoefu wake, kujifunza namna nzuri za uendeshaji wa biashara na kufungua milango mipya ya masoko kupitia kuchangamana na watu wenye biashara tofauti.

“Kampuni zinazoshiriki zinaweza kupata uzoefu na ushauri kutoka kwa kampuni zilizofanikiwa zaidi katika biashara. Ni muhimu kuzileta kampuni hizi pamoja ili waweze kuzungumza wenyewe kuhusiana na yanayoendelea katika soko,” anasema Friend.

Hyatt anasema inatumia kampuni za kati katika usambazaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika katika shughuli za uendeshaji wa hoteli na utashi wao wa kuzisaidia kampuni hizo kukua zaidi ndiyo umewasukuma kushiriki katika Top100 kama wadhamini.

“Hoteli yoyote kubwa kama sisi inahitaji wabia wa kutosha ili iweze kufanikiwa. Unajikuta unahitaji kila kitu kutoka kwa wasambazaji, kuanzia vyakula, magodoro hata wataalamu wa vitu mbalimbali,” anasema Friend.