In Summary

Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ukonga, Mwita Waitara amejigamba kwamba alikuwa mbunge aliyeuliza maswali mengi ya msingi bungeni kuliko mbunge yeyote wa Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa CCM jimbo la Ukonga, Mwita Waitara amejigamba kwamba alikuwa mbunge aliyeuliza maswali mengi ya msingi bungeni kuliko mbunge yeyote wa Dar es Salaam.

Waitara ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wakati akiomba kura kwa wakazi wa Gongo la Mboto ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa mbunge wa jimbo hilo.

Waitara aliyehamia CCM Julai 28, 2018 akitokea Chadema ambako alikuwa mbunge wa Ukonga, amewataka wananchi hao kumchagua ili akawasilishe kero zao bungeni, kwamba kwa kushirikiana na wabunge wa chama tawala pamoja na Serikali anaamini kero zao zitatatuliwa.

"Nikiomba kitu bungeni timu yote ya CCM itaniunga mkono, nikihitaji kitu waziri yeyote atanisikiliza. Ndio maana nimehamia huku (CCM) ili niwe karibu na Serikali kutatua kero zenu," amesema Waitara.

Mgombea huyo ameahidi kwamba atahakikisha anajenga shule ya sekondari Ukonga pamoja na daraja la Mongolandege kabla ya 2020.

Kuhusu shida ya maji, Waitara amesema tayari Serikali imesikia kilio chake na kazi imeanza kuhakikisha kwamba wananchi wa jimbo hilo wanapata maji ya uhakika.

"Baadhi ya maeneo ya jimbo hili yana shida ya umeme, tutakwenda bungeni kuisukuma Serikali kuleta umeme wa Sh27,000 badala ya ule wa Sh300,000. Nichagueni nikalisimamie hili," amesema Waitara.

Waitara amekanusha madai kuwa alinunuliwa ili ahamie CCM huku akisisitiza kuwa wapo viongozi wengi waliohama lakini hawasemi kama walinunuliwa.

"Jana tulipokuwa Msongola, viongozi wa Chadema karibu wote wa kata walirudisha kadi zao, nao wamenunuliwa? Madiwani wa Chadema zaidi ya 200 wamehamia CCM, nao wamenunuliwa?" Amehoji.