In Summary

Kamanda Sabas amesema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani 

Dar es Salaam. Jeshi la polisi Kanda Maalum limewakamata watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu wakiwamo 12 wa mtandao wa wizi wa magari na walioiba viatu vyenye thamani ya Sh 600 milioni.

Akizungumza na wanahabari leo Julai 11, Kaimu Kamanda wa polisi, kanda maalum ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas amesema  Mei 23 polisi walikamata watuhumiwa hao wakiwa na katoni 500 za viatu zenye thamani ya Sh600 milioni zilizoibwa kwenye ghala la kampuni ya Bata Mei, 21.

“Watuhumiwa hao pia walikamatwa na gari aina ya mistubishi canter T 686 BWY ambalo lilikuwa limebeba mizigo hiyo pamoja na katoni 71 za bia mifuko 18 ya sabuni ya unga,injini 4 za pikipiki,na maboksi 61 ya nguo za mitumba”amesema

Kadhalika amesema Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 12 wa mtandao wa wizi wa magari na pikipiki katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam.

Kamanda Sabas amesema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakama

Pia jeshi hilo la polisi limemkamata Omwalimu Binyakusha mmiliki wa Kampuni ya Arise Special Sunrise Safaris kwa kuwatapeli raia wawili wa kigeni.

“Mtuhumiwa huyu alichukua fedha kwa raia hao wa kigeni kwa makubaliano ya kuwapeleka safari lakini mwishoni aliwatelekeza hadi Serikali ilipoamua kuwahudumia,”amesema Sabas.