In Summary

Wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao maeneo ya mpakani mwa nchi za Afrika Mashariki wametaja sababu zinazowakwamisha katika biashara zao.

Kenya. Wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao maeneo ya mpakani mwa nchi za Afrika Mashariki wanadaiwa kuumizwa na uamuzi unaofanywa na baadhi ya nchi hizo.

Hali hiyo inatajwa kuwafanya washindwa kunufaika na kutumia fursa zinazojitokeza ndani ya soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CM) ambalo limefungua milango ya usafirishaji huru wa bidhaa, huduma na mambo mengine ya biashara.

Wakizungumza katika mafunzo ya kuwanoa wakufunzi kuhusu mwongozo wa wafanyabiashara wadogo na wanawake maeneo ya mpakani, wamesema mabadiliko ya ushuru wa forodha na uwepo wa katazo la mara kwa mara miongoni mwa nchi wanachama ni kikwazo kwao.

 “Wafanyabiashara wadogo wanawake na makundi ya watu yasiyo na fursa ndiyo wajasiriamali wakubwa, ndio wanaotarajiwa kuwa wanufaikaji wakubwa kama EAC ingejitahidi kupanua wigo wa utoaji elimu kuhusu sheria za mipakani,” amesema Dk Kirsten Focken, kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GTZ) anayehusika na masuala ya EAC.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa mpakani Kenya, Florence Atieno amesema uamuzi unapofanywa na baadhi ya nchi wanachama taarifa zake haziwafikii wafanyabiashara kwa wakati muafaka.

Amesema hali hiyo inasababisha hasara kwa vile hulazimika kutumia fedha nyingi kukidhi mabadiliko hayo.

Atieno ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha kuweka na kukopa chenye wanachama 600, amesema Serikali za nchi wanachama zinapaswa kuwafahamisha mapema wafanyabiashara waliopo mipakani ili kuepuka kuathiri shughuli zao.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, mwenyekiti wa chemba ya biashara ya wanawake mkoani Kilimanjaro (TWCC), Joyce Ndossy ameeleza jinsi wakulima wa mahindi Tanzania wanavyoumia kutokana na uamuzi wa ghafla ya upigaji marufuku usafirishaji wa mahindi nje.

“Kwa sasa gunia moja la mahindi Tanzania linauzwa kati ya Sh18,000 na Sh25,000,” amesema Ndossy na kubainisha kuwa hali hiyo isingetokea kama Serikali isingepiga marufuku usafirishaji huo.

“Mara tu Serikali yetu ilipopiga marufuku wafanyabiashara wa Kenya walihamia katika soko la Comesa. Waliingiza mahindi kutoka Malawi, Uganda na Zambia. Mpaka tunabaini bei ya gunia la mahindi ilikuwa imeshuka.”