In Summary

Wabunge walijadili kwa upana suala hilo bungeni lakini kulikuwa na zomea zomea.

Dodoma. Unaweza kusema hoja ya watu kutekwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha imechafua hali ya hewa bungeni baada ya wabunge wa CCM na upinzani kuzomeana wakati wakijadili hoja hiyo iliyoibuliwa bungeni leo Jumatatu Aprili 16, 2018 na mbunge wa Mtambili (CUF), Masoud Abdalla Salim.

Mbunge huyo alihoji sababu za watu kutekwa akitolea mfano watu sita waliotekwa siku za hivi karibuni visiwani Zanzibar wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mwaka 2018/19. Hata hivyo watu hao wameshapatikana.

Salim amesema yupo tayari kumpa namba za gari Waziri wa ofisi hiyo, George Mkuchika na kutaka jambo hilo kujadiliwa bungeni.

Zomea zomea hiyo ilianza baada ya mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia kuanza kuchangia hoja hiyo na kuipinga akibainisha kuwa  jambo hilo linazungumzwa lakini halina ukweli wowote.

“Huo ndio ukweli wenyewe. Hili jambo si kweli. Suala la usalama ni nyeti sana, kama namba ya gari unazo tutahakikisha vipi kama ni zenyewe. Hoja hii haina msingi naungana na maelezo ya Serikali,” alisema Mtulia ambaye alikuwa mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF kabla ya kuhamia CCM Desemba mwaka jana, chama hicho kumpitisha kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Aliposimama mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Magereli kuanza kuchangia hoja hiyo, baadhi ya wabunge wa CCM walianza kumzomea jambo ambalo Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alilipinga na kuwaonya wabunge kuwa huo si utaratibu wa kibunge.

Katika maelezo yake, mbunge huyo wa Chadema amesema usalama wa raia kwa sasa si mzuri, kwamba kumekuwa na matukio mengi ya utekaji na kutaka kauli ya Serikali kudhibiti matukio hayo.

Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga amesema hata mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amewahi kutishiwa bastola na mtu aliyehusishwa na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) lakini mpaka leo hakuna kauli yoyote iliyotolewa kukanusha suala hilo.