In Summary
  • Serikali imesema baada ya kibano cha wabunge kuhusu mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa muda wa wiki mbili imetolewa Sh 13 bilioni huku wakurugenzi wakitakiwa kufikisha asilimia 100 ya utekelezaji wa utoaji wa mikopo ifikapo Julai 20 mwaka huu

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema baada ya kikao cha wabunge na wakurugenzi Tanzania wiki mbili zilizopita, Sh13 bilioni zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Aprili 15, 2019, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) Seleman Jafo wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi yake.

Amesema suala la utoaji wa mikopo limekuwa na changamoto kubwa sana hasa utoaji wa asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Amesema Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 ilifanyiwa marekebisho inaelekeza namna ya kutoa fedha hizo kwa mujibu wa sheria.

“Naishukuru sana Kamati ya Bunge ya  Serikali za Mitaa na Utawala ilikutana wakuu wa mikoa wote kupitisha bajeti hoja mahususi ambayo ilijadiliwa kwa mapana zaidi,” amesema.

Amesema kwa wiki mbili Sh13 bilioni  zimetolewa na hadi kufikia Machi 30 Sh 20.7 bilioni zimetoa na hivyo kufikia asilimia 38.7 utekelezaji wake.

Amesema kanuni zimeshatoa kwa ajili ya suala hilo na amewataka maofisa masuhuli (wakurugenzi) mikopo itakapofika Juni 28 mwaka huu asilimia 83.3 ya mkopo iwe imetolewa.

Amesema Julai 20 mwaka huu, asilimia 100 wawe wametoa asilimia 100 ya mikopo hiyo na wakurugenzi watakaoshindwa  kuna utaratibu wa kisheria utachukuliwa.

“Si rahisi kuna mkurugenzi anataka kuingia kikaangoni mikopo hii ni haki ya vijana ambao wamekosa ajira,” amesema.