In Summary
  • Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu usalama barabarani 2018, inaeleza kwamba majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ndiyo chanzo kikubwa kinachoongoza kwa vifo vya watoto na vijana wa kati ya umri wa miaka mitano hadi 29 kwa sasa.

Geneva, Uswisi. Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika kukabiliana na changamoto ya usalama barabarani ulimwenguni.
Katika ripoti hiyo mpya iliyozinduliwa wiki hii mjini hapa, WHO inasema vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vinaendelea kuongezeka na kufikia 1.35 milioni kwa mwaka.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la 'Mtazamo wa kimataifa wa WHO kuhusu usalama barabarani 2018' inaeleza kwamba, majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ndiyo chanzo kinachoongoza kwa vifo vya watoto na vijana wa kati ya umri wa miaka 5 hadi 29 kwa sasa.
Akisisitiza haja ya kukabiliana na tatizo la ajali hizo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema: “Vifo hivi ni gharama isiyokubalika katika safari, hakuna kisingizio chochote kwa kutochukua hatua, hili ni tatizo ambalo lina suluhu. Ripoti hii ni wito kwa Serikali na wadau wote kuchukua hatua zaidi kutekeleza mikakati hiyo.”
Ripoti hiyo pia imesema licha ya idadi ya vifo kuongeza, kiwango cha vifo kulingana na idadi ya watu duniani kinaonekana kutokuwa kikubwa sana kwa miaka ya karibuni, hii ikiaashiria kwamba juhudi zilizopo za usalama barabarani katika nchi za kipato cha wastani na kipato cha juu zimesaidia.