Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Kilimanjaro, imewafikisha mahakamani vigogo wawili wa zamani wa halmashauri ya wilaya ya Rombo mkoani humo kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh95 milioni.

Waliofikishwa mahakamani leo Alhamisi Novemba 8, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Regina Futakamba ni aliyekuwa mhasibu wa halmashauri hiyo, Robert Msuka na ofisa utumishi, Edson Mkondora.

Msuka ambaye sasa ni mhasibu wa halmashauri ya Misenyi na Mkondora ambaye sasa ni ofisa utumishi wa halmashauri ya Siha, waliunganishwa na watuhumiwa wengine wawili katika kesi hiyo.

Watuhumiwa waliounganishwa nao ni Veneranda Mosha ambaye kwa sasa ni Mtunza Fedha wa halmashauri ya wilaya ya Rombo na Godfrey Mwakalinga, aliyekuwa dereva wa halmashauri hiyo.

Katika shitaka la kwanza, Mkondora, Msuka na Veneranda, wanashitakiwa kwa kutumia nyaraka za udanganyifu kuonyesha Sh67.2 milioni zilitumika kukodi magari katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Nyaraka walizowasilisha kuhalalisha matumizi ya fedha hizo, zilionyesha namba za magari ya Serikali, malori, pikipiki na namba ambazo haziko kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, ilidai pia wameshitakiwa kwa kutumia nyaraka za uongo, kuwa Sh8.6 milioni zilitumika kwa matangazo.

Mwendesha mashitaka wa Takukuru, Rehema Mteta alidai katika kipindi hicho, waliwasilisha nyaraka za udanganyifu kuwa Sh18.4 milioni zilitumika kwa ajili ya chakula na viburudisho.

Katika shitaka pekee linalomkabili Mwakalinga, mwendesha mashitaka huyo alidai mshitakiwa huyo ambaye hakuwepo kortini, alitoa nyaraka za udanganyifu kuwa Sh575,565 zilitumika kununua mafuta ya dizeli.

Washitakiwa hao wamekana mashtaka yao na mahakama imetoa hati ya kuitwa mahakamani kwa mshitakiwa Mwakalinga ambaye tayari alishaachishwa kazi katika halmashauri ya wilaya ya Rombo.