In Summary
  • Tanzania ni moja ya nchi 10 duniani zenye kiwango cha juu cha vifo vya watoto ikitanguliwa na India, Pakistani, Nigeria, Congo, Indonesia na Afiganstan.

Dar es Salam.  Watoto 312 wenye umri chini ya miaka mitano hupoteza maisha kila siku kutokana na magonjwa yanayoweza kutibika kama malaria, nimonia na kuhara.

Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Tahseen Alan amesema vifo hivyo vya watoto ni sawa na ujazo wa abiri kwenye mabasi madogo 10 ya aina ya Toyota Coaster   zenye uwezo wa kubeba abiria 32 zianguke na kuua abiria wote kila siku.

Tahseen ametaja takwimu hizo leo Ijumaa Machi 24, 2019 alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu kampeni ya Jiongeze, ‘Tuwavushe Salama’,  inayolenga kuzuia vifo vya mama na mtoto.

Kampeni hiyo inatekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Kampuni ya ya True Vision na Unicef.

Amesema vyombo vya habari vinalo jukumu kubwa la kuhakikisha jamii inafahamu mengi kuhusu huduma za afya hasa ya mama na mtoto.

Ofisa Habari wa Unicef nchini, Usia Nkoma amesema Tanzania ni kati ya nchi 10 duniani zenye kiwango cha juu cha vifo vya watoto.

“Na asilimia 50 ya vifo hivyo vinatokea ndani ya mwezi mmoja wakati asilimia 40 kati ya hiyo, 50 hutokea saa moja baada ya kuzaliwa,” amesema Nkoma.

Amesema siku moja hadi 30 ni muhimu kwa uhai wa mtoto na kwamba, lazima kushirikiana ili kuhakikisha Tanzania inatoka kwenye orodha hiyo kwa kuufanya uzazi kuwa salama.

“Vifo hivyo vinatokana na sababu zinazoweza kuzuilika, kuzaa halipaswi kuwa suala la kufa na kupona, kuzaa lazima liwe jambo salama, isiwe mama akiingia kujifungua basi ndugu wanabaki na hofu atapona au laa,” amesema.

Awali, Kaimu Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Agness Mgawa alisema inawezekana kabisa kuokoa vifo vya mama na mtoto kama kila mtu atashiriki.

Amesema sababu za mkakati wa Serikali ni kuokoa vifo vya watoto 43 kwa kila vizazi 1,000 na kufikia 25 kwa kila vizazi 1,000.

Naye mtaalamu kutoka True Vision, Isack Lukando anasema elimu kwa jamii itasaidia kupunguza vifo hivyo na kuviomba vyombo vya habari kulifanya suala la uhai wa mama na mtoto kuwa ajenda.

“Kila mtu aone suala la uhai wa mama na mtoto linamuhusu na ashiriki kuokoa uhai wake, mara nyingi huwa inaonekana kama haiwezekani lakini mtu akiamua kufanya inawezekana, kwa hiyo inawezekana kabisa kila mtoto anayezaliwa na mama anayejifungua wote wakawa hai,” anasema Lukando.