In Summary

Wanamuziki hao walionyesha uwezo mkubwa wa kutawala jukwaa na kuleta burudani ya pekee.

Mwanza. Wanamuziki nyota wa kizazi kipya nchini, Vanessa Mdee na Juma Jux wameanza kwa vishindo ziara yao ya kimuziki ijulikanayo kwa jina la “In Love with Money”.

Ziara hiyo imeandaliwa na wanamuziki hao kwa lengo la kumpromoti muziki wao wa kizazi kipya na mbali ya Mwanza, pia mikoa ya  Mtwara, Dodoma, Arusha na Dar es salaam watapata uhondo huo.

Katika shoo iliyofanyika kwenye viwanja vya Rock City Mall, na kuhudhuriwa na washabiki zaidi ya 5,000, wanamuziki hao walionyesha uwezo mkubwa wa kutawala jukwaa na kuleta burudani ya pekee.

Wimbo ambao uliwavutia sana mashabiki ilijulikana kwa jina la Juu ambao wanamuziki hao walitawala jukwaa kwa kukonga nyoyo za mashabiki. Mbali ya wanamuziki hao, pia wasanii wengine wa  muziki wa kizazi kipya walipamba onesho hilo.

Nyota wa muziki huo hasa katika miondoko ya Hip Hop, Stamina, naye alifanya shoo katika tamasha hilo. Stamina alifanya ‘Surprise’ katika shoo hiyo pamoja na kutokuwepo katika ratiba.

Wanamuziki hao sasa wataelekea Mtwara Jumamosi ijayo na baadaye Julai 14 watakuwa Dodoma kabla ya kufanya shoo nyingine Arusha Julai 21. Wakazi wa Dar es salaam watapata raha za shoo za wanamuziki hao Julai 28.