In Summary

Serikali imesema itafanya hivyo kutokana na ripoti ya CAG kueleza kuwa deni hilo limeongezeka kwa kipindi cha miezi sita


Dodoma. Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo inafanyia tathimini deni la matibabu ya nje ya nchi ili kujua uhalali wake.

Kwa mujibu wa Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 limeongezeka kwa Sh 17.13 bilioni kwa kipindi cha miezi sita.

CAG amesema deni la gharama za matibabu ya nje ya nchi katika hospitali za India limeongezeka kutoka Sh 28.60 bilioni kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka 2017 hadi kufikia Sh 45.73 bilioni kufikia Desemba 30 mwaka 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 17, 2018 mjini Dodoma, Ummy amesema utaratibu unaotumika kulipa deni la matibabu ya nje ya nchi ni utaratibu madai hayo kupelekwa  kwenye ofisi za ubalozi wa India.

Amesema mara baada ya kupokea madai hayo ubalozi hufanya uhakiki wa awali kabla ya kuyapeleka wizarani. Amesema wizarani kupitia madaktari bingwa hufanya uhakiki ili kujiridhisha usahihi wake kwa kurejea matibabu yaliyokusudiwa, yaliyofanyika na gharama husika kwa kadri ya mkataba na bei za matibabu.

“Wizara inatambua kuwa deni la matibabu ya wagonjwa nje ya nchi ni kubwa na hii ni kwa kuwa, ulipaji wake umekuwa ukifanyika kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na siyo kwa kadri ya deni inavyohakikiwa,” amesema.