In Summary

Ametoa kauli hiyo katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2018/19

Mbunge wa Mtama (CCM),  Nape Nnauye ameitaka Serikali kutoona aibu kuiondoa bungeni bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2018/19 ili ikajipange upya kwa maelezo kuwa bajeti hiyo itaiumiza Serikali ya Awamu ya Tano.

Nape pia amehoji zilipo fedha ambazo Serikali imekuwa ikijigamba kuwa imekusanya kwa kiasi kikubwa wakati hakuna fedha katika miradi ya maendeleo.

Nape ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 16, 2018 wakati akizungumza katika mjadala wa bajeti hiyo bungeni mjini Dodoma.

Waziri huyo wa zamani wa habari amesema umefika wakati wa kueleza ukweli kuwa bajeti ya wizara hiyo ni ngumu na haiendani kabisa la Ilani ya uchaguzi ya CCM, ikipitishwa itakuwa mwiba kwa Serikali.

Amesema anamuonea huruma Waziri wa Kilimo,   Dk Charles Tizeba kwa maelezo kuwa kuna mambo yaliyo nje ya uwezo wake, lakini kila jambo anabebeshwa yeye.

“Ni mtihani mkubwa kwa Serikali katika bajeti ambayo inagusa asimilia 80 ya Watanzania. Bajeti hii inagusa maisha ya watu hivyo ujumbe unaotakiwa kwa wananchi ni je, Serikali inajali maendeleo ya vitu au watu waliowaweka madarakani jambo ambalo majibu yake yatakuwa na maana tofauti kwa wananchi.”

Amesema Serikali haiwajali  wakulima kwa maelezo kuwa imekuwa ikipunguza bajeti hiyo kuanzia mwaka 2018/17.

“Wakati fulani tulisema Serikali ikwepe kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa inayoweza kujiendesha kibiashara, lakini tukashambuliwa kama si wazalendo katika nchi hii, na hili Tizeba tutakubebesha bure lakini si lako,” amesema Nape.

Amesema akikubali bajeti hiyo, wananchi wake wa Mtama na wakulima wa korosho, ufuta, pamba na mazao mengine nchini watamshangaa kwa kiasi kikubwa hivyo hakuna shida wala aibu kukaa pamoja na kuifumua kama ilivyowahi kufanyika kwa wizara nyingine.

Alisema Ilani ya uchaguzi wa CCM ilitamka kuwa Serikali itakayoundwa itakuwa na jukumu la kuwasaidia wakulima kutafuta masoko ya nje lakini kwa sasa imekuwa kinyume kabisa na ilani hiyo, kwamba kukaa mezani ndio suluhu.

“Ukimwambia mtu akale magunia 20 ya mbaazi si unamtukana huyu, hivi tunawaambia nini wakulima katika jambo hili, ni kwa nini tusiwe wepesi wa kukubali ushauri na kuzungumza kwa pamoja,” amehoji.