In Summary
  • Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo ametua mkoani Njombe kufuatilia matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyoanza mwishoni mwa Novemba 2018

Njombe. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo ametua mkoani Njombe kufuatilia matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyoanza mwishoni mwa Novemba 2018.

Amesema amefika Njombe kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini Tanzania hivyo katika matukio hayo vyombo vyote vinashirikiana.

Leo asubuhi Jumatatu Februari 11, 2019 amefanya kikao cha ndani na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Njombe pamoja na vikosi maalumu vilivyopo mkoani humo kuchunguza matukio hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mabeyo amesema sababu za utekaji na mauaji ya watoto  yanahusisha zaidi ngazi ya familia na vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza kuchukua hatua kukomesha mauaji hayo.

“Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa kushirikiana pamoja na jeshi. Na mimi ndiye mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi hivyo ninaowajibu na si kwamba jeshi limeingia sasa, hapana hatujafikia hatua ya kuingiza jeshi,” amesema Mabeyo.

"Wananchi karibu nchi nzima wamesikia kinachoendelea Njombe.  Wengine yamewatia hofu lakini si Tanzania tu mpaka nje ya mipaka yetu taarifa zimesambaa,” amesema.

Ameongeza, “Sisi kamati ya ulinzi na usalama baada ya matukio tulileta timu maalumu mapema ishirikiane na vyombo vilivyopo huku (Njombe) katika kufanya uchunguzi makini na wa kina.”

Amewataka wananchi kutulia kwani vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake vizuri kuhakikisha waliohusika wanabainika, akisisitiza kuwa sababu ya kutekeleza mauaji hayo zinafahamika na kwamba taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

“Kwa hiyo pasiwepo na hofu suala hili ni la kitaifa zaidi, hapana,  linahusu pengine familia moja moja sababu zinajionesha kabisa ni za kifamilia zaidi,” amesema.

“Sasa kama ni za kifamilia ni lazima itafutwe njia ya kuzuia au kudhibiti matukio kama haya yasiendelee kwa watu wengine.”

Amesema suala hilo lazima litakomeshwa na si Njombe pekee bali nchi nzima katika maeneo mengine yenye matukio kama hayo kwa imani potofu kwa wananchi zilizotaka kuanza kujengeka.

Amewataka wananchi kuendelea kufanya kazi zao kama kawaida kwa maelezo kuwa vyombo vya Dola vinatekeleza majukumu yake kama kawaida.

Amesema vyombo vyote vinashirikiana kwanza kujua ni kina nani waliohusika, sababu za kuhusika na mbinu zilizotumika huku akibainisha mbinu zilizotumika na watekelezaji wa mauaji hayo ni za kawaida na hazihitaji jeshi kufanya kazi hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga amesema hadi sasa watuhumiwa 30 wanashikiliwa kutokana na kuhusika kwao na utekaji na mauaji ya watoto hao.

Alisema jalada la watuhumiwa hao lipo kwa mwanasheria na muda wowote watafikishwa mahakamani.