In Summary
  • Mhandisi wa kivuko cha MV Nyerere anasema kumbukumbu ya ajali ya kivuko hicho inaendelea kumtesa. Hii imemlazimu kuwa kwenye kundi la watu wengi na nyakati za usiku anafanya mazoezi.

Mwanza. Licha ya kunusurika kwa ajali ya MV Nyerere iliyowaangamiza watu 230, fundi mkuu wa kivuko hicho Alphonse Charahani anaendelea kuteseka na kumbukumbu ya ajali hiyo.

Ili kukabiliana na kumbukumbu mbaya ya tukio hilo, anahakikisha kwamba kila wakati anakuwa na watu wa kuzungmuza naye na inapotokea yupo pekee yake hujishughulisha kwa kufanya mazoezi hata ya kurukaruka ndani na kukimbia kuzunguka kwenye ua na makazi ya familia yake yaliyopo, Kifongo Feri, wilayani Misungwi.

“Mara nyingi nikiwa peke yangu nateseka sana naingiwa na hofu kubwa hususan nikikumbuka ajali ile ilivyotokea na idadi ya watu walioangamia kwenye kivuko,” amesema Charahani.

Mhandisi huyo amesema haipiti dakika moja kabla hajakumbuka marafiki na wafanyakazi waliokuwemo kwenye kivuko.

Anasema mara nyingi akiwa bafuni au sehemu nyingine peke yake, anaingiwa na huzuni mkubwa akijiwa na kumbukumbu ya tukio hilo.

Ameelezea kwamba wakati mwingine inabidi adanganye watu sehemu alipo ili kupata muda wa kupumzika na kuendelea kuwa na marafiki na majirani zake wanaomfariji.

“Siku hizi, simu yangu wala haikai na ‘chaji’, inapigwa muda wote hata usiku wa manane. Ni vigumu kushindwa kuipokea na wakati mwingine nalazimika kudanganya hasa kwa wale wanaotaka kuja kunihoji,” amesema.

Maisha

Ameelezea kwamba ndugu na watu wake wa karibu wameanza kuingiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na yeye kubadilikabadilika kila wakati.

“Mimi mwenyewe najikuta nimeingiwa na simanzi. Kitendo cha ajali ile nahisi kimeniathiri sehemu kubwa ila nazidi kumuomba Mungu ili nirudi hali yangu ya kawaida,” amesema mhandisi.

Anasema licha ya kwamba hana mpango wa kuiacha kazi yake ya uhandisi, anahisi itamchukua muda mrefu kusahau tukio hilo na daima ataendelea kumuomba Mungu wake.

Kwa sasa mhandisi huyo anasema anapata wageni wengi nyumbani kwake, miongoni mwao, wakiwa kutoka mikoa ya mbali na wenyeji pia.

“Kila mtu anataka nianze upya namna ajali ile ilivyotokea. Nahisi huzuni na uchungu mkubwa sana kwa kweli,” mhandisi Charahani.

Siku ya ajali

Manusura huyo wa ajali, anasema akiwa chini ya kivuko kile kikiwa kimepinduka, aliiwaza familia yake kwamba hakuwa amewaaga na pia hakutarajia kufariki siku ile bila ishara yoyote ya kuugua.

“Mimi ni baba wa watoto wanne na mke mmoja, mwanangu wa kwanza yupo chuo,wawili sekodari na huyu wa mwisho yupo darasa la tatu. Kiukweli nililia sana na niliamini kabisa kwamba maisha yangu yamefika tamati,” anasimulia mhandisi.

Anasema akiwa pale ndani, alisikia kama sauti za binadamu zikiwa upande wa juu wa kivuko hicho lakini mbinu na jitihada za kuwasiliana nao zilikuwa ni ngumu sana.

Mzamiaji anena

Mmoja wa wataalamu walioshiriki zoezi la uokoaji katika ajali ya MV Nyerere, Fakhi Mbarouk, alieleza jinsi chupa ya chai ilivyoweza kubaini uwepo wa mhandisi wa kivuko akiwa hai zaidi ya masaa 48 tangu kilipopinduka.

Mmbarouk anasema haikuwa rahisi kumuokoa mhandisi kwani alikuwa eneo lisilofikika kirahisi ndani ya kivuko hicho.

Mtaalamu wa kikosi cha wazamiaji, Zanzibar anasema hofu na woga wa fundi huyo dhidi ya viumbe wa majini pia ilikuwa moja ya changamoto walizokumbana nazo.

“Tulipata uhakika kwamba mhandisi alikuwa hai kwani alikuwa akikimbiza miguu mara tu tulipomgusa, nadhani alihisi kwamba ni viumbe vya majini,” anasema mwenyekiti huyo wa chama cha waogeleaji, Zanzibar.

Muokoaji huyo anasema walimtumia chupa ya chai na ujumbe wa maandishi kwenye karatasi wakimueleza kwamba awe mtulivu wakimhakikishia kumuokoa.

“Alikunywa chai ile na kurejesha chupa kupitia upenyo ule ule tuliotumia kumpitishia. Kitendo cha yeye kunywa chai na kurejesha chupa, tulijiridhisha kwamba yupo hai na tukaazimia kwamba lazima tumuokoe,” alisema Mbarouk

Afya

Baada ya mhandisi kuokolewa Septemba 22, 2018 na kukimbizwa hospitali. Alipata huduma katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza na baadaye kuruhusiwa.

Anasema kwa sasa kinachomsumbua ni kumbukumbu ya ajali ile lakini mwilini mwake anahisi yupo sawa kwani maumivu aliyokuwa nayo yanaendela kutokomea, hatua kwa hatua.

Mhandisi huyo anatarajia kurejea Hospitali ya Bugando kesho (Ijumaa),kwa ajili ya uchunguzi kama alivyoelekezwa na madktari.

Hatua

Mhandisi ameelezea kwamba kati ya watu 41 walionusurika kwenye ajali hiyo, wafanyakazi akiwemo yeye walizuiliwa na kufanyiwa mahojiano maalumu na vyombo vya sheria na kumshukuru Mungu kwamba yeye alimalizana na tuhuma zote salama.

Amesema kwamba, nahodha wa MV Nyerere, Omari Ngwenye na mabaharia wawili, bado wanashikiliwa na polisi jijini Mwanza.

“Mimi nilipoitwa kwenye tume ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri Mkuu niliingiwa na wasiwasi lakini nashukuru Mungu, baada ya kujieleza wengi walinielewa,” mhandisi Charahani.