In Summary

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo na ambaye awali alikuwa mbunge wa Kigoma Vijijni kwa tiketi ya Chadema, ataweza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao baada ya klufikisha umri unaotakiwa kisheria.

 


Dar es Salaam. Kuna watu wamekuwa wakiishi kwenye ndoto, wapo wanaotamani kuwa madaktari, wapo waliotamani kuwa wachezaji, lakini Zitto Kabwe anawazia urais, na haishii hapo, bali anaeleza hali itakavyokuwa atakaposhika nafasi hiyo ya juu kisiasa.

“(Wananchi) Mtachapa kazi, lakini mtakula bata (mtastarehe),” ameandika kiongozi huyo wa ACT Wazalendo katika akaunti yake ya Twitter.

Kauli hiyo imeibua mijadala mtandaoni huku wachangiaji wakiuliza zaidi jinsi atakavyoendesha mwanasiasa huyo nchi.

“Ninaamini nitakuwa rais bora kwa uwezo wake Mola. Nitauona upinzani kama chachu ya maendeleo badala ya kuwa na hofu nao,” anasema Zitto.

“Nitarejesha taswira chanya ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa kwa kulinda demokrasia na haki za binadamu. Mtachapa kazi, Lakini pia mtakula bata,” amesema Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.

Mwanasiasa huyo kijana amesema katika uongozi wake, atamteua Fatma Karume ambaye sasa ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kumsaidia kwenye mabadiliko ya mfumo wa utoaji haki.

“Nitamteua @fatma_karume kusimamia mabadiliko makubwa ya mfumo wa utoaji haki nchini ili kukomesha vitendo vya uonevu na ukatili,” amesema.

“Kwa matendo ya nyuma tutaunda Tume ya Ukweli na Maridhiano ili wahanga wajitokeze kwa uwazi na wahusika wa matendo haya wahukumiwe na umma #KaziNaBata,” amesema

Fatma Karume hakuwa mbali na kuitikia wito huo kwa kumjibu Zitto akisema, “@zittokabwe Kazi ya ku-chair (kuwa mwenyekiti wa) Tume ya ku-investigate (kuchunguza) na kutoa mapendekezo ya kubadilisha mfumo wa utoaji haki including namna ya kuwachagua watoa haki; fundamentals ya utoaji haki ni is a job I would truly relish. And I thank you for considering me for that job (ni kazi ambayo ningeifurahia na nakushukuru kwa kufikiria kunipa nafasi hiyo).”

Zitto Kabwe alizaliwa Septemba 24, 1976 katika Kijiji cha Mwandiga mkoani Kigoma na wakati siasa za ushindani zinarejeshwa nchini mwaka 1992, alijiunga na Chadema. Aligombea ubunge wa Kigoma Kaskazini mwaka 2005 na kushinda na hivyo kushikilia nafasi hiyo hadi mwaka 2015 alipohamia Kigoma Mjini.

Hata hivyo, hali yake haikuwa nzuri ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani baada ya kutuhumiwa kutaka kumuondoa mwenyekiti Freeman Mbowe, lakini kabla ya chama hakijamchukulia hatua, alikwenda mahakamani kukizuia kumzungumzia hadi shauri kuu alilokuwa amelifikisha katika chombo hicho la uhalali wa uanachama wake litolewe uamuzi.

Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubaliana na hoja za Chadema kuwa hakufuata taratibu wakati wa kufungua kesi hiyo na muda mfupi baada ya uamuzi huo, chama hicho kikatangaza kumtimua.

Mara kadhaa Zito amekuwa akizungumzia ndoto zake za kushika nafasi ya juu ya kisiasa nchini licha ya kupitia matatizo kadhaa na amekuwa akieleza kuwa ataweza kufanikiwa kama ilivyokuwa kwa waziri mkuu wa zamani wa India, Indira Gandhi.

Na leo alipata nafasi ya kuulizwa maswali kuhusu urais wake ujao.

Mmoja wa wanaomfuata kwenye akaunti hiyo, Magembe Herrera aakamuuliza kuhusu ‘fao la kujitoa’, moja ya mambo yanayojadiliwa sana baada ya Serikali kutangaza kanuni za mifuko ya jamii.

“Kuhusu fao la kujitoa kwa tunaofanya kazi za mikataba na mafao ya uzeeni je?” amehoji Herrera.

Na Zitto aakamjibu: “Wafanyakazi wa mikataba watakuwa na scheme (mfuko) maalumu ambayo itawafanya wachukue akiba zao bila kuathiri mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii. Itakuwa ni marufuku Mtanzania kutokuwa na Hifadhi ya Jamii. Wasio na uwezo watawezeshwa na Serikali wawe na uwezo wa kuweka akiba #KaziNaBata.”

Mchangiaji mwingine, Kaila (Mwenzetu) naye akamuuliza Zitto kuhusu uhuru wa kutoa maoni, kumshauri na kukukosoa iwapo atakuwa rais na kama itakuwa lazima kwake kuungwa mkono na watu wote.

“Nitahakikisha Katiba inasimamiwa mpaka nukta na kila raia atakuwa huru kukosoa Serikali yetu. Tutatumia ukosoaji kuboresha kazi zetu. Tutalinda Uhuru wa kujieleza na Uhuru baada ya kujieleza #KaziNaBata,” amesema Zitto.

Mchangiaji mwingine katika hoja hiyo, Frank J Masemele akamgeuzia kibao.

“Acha uongo wewe. Wachapakazi hawana muda wa kula bata. Chagua moja, bata ama kazi. Halafu ndoto zako bwana. Dah,” ameandika Masemele.

Na Zitto hakumuacha.

 “Wewe labda! Watanzania wamechoka wanataka #KaziNaBata,” amesema Zitto.