In Summary

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa upelelezi wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi upo katika hatua za mwisho


Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi upo hatua za mwisho.

Watuhumiwa sita wanaokabiliwa na mashtaka hayo ya mauaji ya Dk Mvungi waliachiwa na Mahakama Kuu Novemba 22, 2018  na kufunguliwa shtaka kama hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao  ni Msigwa Matonya (35), Mianda  Mlewa (45), Paulo Mdonondo (35), Longishu Losindo (34), Juma Kangungu (34) na John Mayunga(60

Wakili wa Serikali,  Kija Luzungana ameeleza hayo leo Alhamisi Desemba 6, 2018  mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando kuwa wanakamilisha upelelezi pamoja na kuandaa mashahidi.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo Hakimu Mmbando ameutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati ili washtakiwa waweze kujua hatima yao.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 2O, 2018  itakapotajwa tena na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji kutokuwa na dhamana.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 6, 2018,  washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, 2013 walifanya kosa la mauaji ya kukusudia  kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo  ya tukio katika eneo la Msakuzi Kiswegere Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk  Mvungi.