In Summary

Issack Hassan, aliyeongoza IIEC (baadaye IEBC), aliondolewa  pamoja na wenzake mwaka 2016, walipoandamwa na madai ya ufisadi.


Nairobi. Macho yote sasa yameelekezwa kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati na makamishna wawili waliobaki kwenye tume hiyo baada ya wenzao kujiuzulu jana.
Viongozi mbalimbali wamesema Chebukati naye ajiuzulu pamoja na makamishna Boya Molu na Prof Abdi Guliye, sawa na Naibu Mwenyekiti Consolata Nkatha Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya walivyojiuzulu jana.
Maina na wenzake walimshutumu  Chebukati, na kusema ameshindwa kuongoza tume kwa uthabiti.
“Katika uongozi wake, tume imegeuka kuwa kitengo cha kusambaza habari za kupotosha, kutoaminiana na kujitakia makuu ya kibinafsi,” wamesema hayo kwenye taarifa iliyosomwa na Bwachanya

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen, na mwenzake wa Wachache, James Orengo, wamesema  hatua ya makamishna kujiuzulu ni ishara tosha ya uozo uliopo  IEBC.
Murkomen amewapa makamishna hao siku saba waondoke la sivyo bunge lipewe nafasi ya utendaji kazi wao.
“Wito wangu kutaka makamishna wa IEBC wajiuzulu unatokana na mizozo ya hivi majuzi. Inaonekana mwenyekiti hajawahi kuwa msimamizi awali kabla ya kuchaguliwa kusimamia IEBC,” amesema seneta huyo wa Elgeyo Marakwet.
Kwa upande wake, Orengo amesema : “Hakuna cha makamishna wema wala wabaya waliopo  IEBC. Asasi hiyo ina laana. Kujiuzulu kwa makamishna ni dalili ya maradhi yasiyotibika yanayoikumba tume hiyo.”
Endapo makamishna wote wataondolewa , Kenya itakuwa ikiendeleza mtindo wa kuondoa makamishna wa tume za uchaguzi madarakani  kabla ya muda wao kukamilika, tangu Uchaguzi Mkuu wa 2007.
Katika mwaka wa 2008 makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) wakiongozwa na marehemu Samuel Kivuitu, waliondolewa wakati bunge lilipounda Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Issack Hassan, aliyeongoza IIEC (baadaye IEBC), aliondolewa  pamoja na wenzake mwaka 2016, walipoandamwa na madai ya ufisadi.