In Summary
  • Umri wa mshtakiwa wakwamisha kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha kuendelea kusikilizwa

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kuisikiliza kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha baada ya kubainika miongoni mwa washtakiwa watatu wanaokabiliwa na kesi hiyo, mmoja wao ni mtoto.

Washtakiwa  wanaokabiliwa na kesi hiyo ya jinai namba 675/18 ni Mohammed Mkasi (19) mkazi wa Buguruni Madenge; Abdallah Kwangala (20) mkazi wa Vingunguti kwa Simba; na Jackson Amos (16) mkazi wa Mabibo Farasi. 

Hatua hiyo imefuatia baada ya maelezo ya wakili wa serikali, Aziza Mhina leo Jumatatu Aprili 15, 2019 kuieleza Mahakama kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na kwamba wana mashahidi wawili na wapo tayari kuendelea.

Baada ya Mhina kueleza hayo, Hakimu Flora Mujaya anayeisikiliza kesi hiyo amesema mshtakiwa mmoja katika kesi hiyo ni mtoto. “Hamjaifahamisha Mahakama chochote kuhusu hilo mnaleta mashahidi,” amesema hakimu.

Hakimu Mujaya amesema kabla ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo, lazima upande wa Serikali waieleze Mahakama sheria inavyotaka mtoto anaposhtakiwa pamoja na wakubwa.

Wakili Mhina ameiambia Mahakama kuwa bado suala hilo lilikuwa halijafanyiwa kazi hivyo anaomba wapewe ahirisho fupi ili kulifanyia kazi suala hilo.

Kufuatia hali hiyo, Hakimu Mujaya  imeahirishwa kesi hiyo hadi Aprili 24, 2019.

Katika  kesi hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Septemba 25, 2018 Buguruni Mnyamani  wilaya ya Ilala waliiba simu aina ya Techno yenye thamani ya Sh200,000 na fedha taslimu Sh80,000, mali ya Elizabeth Florian.

Kabla ya kutenda uhalifu huo, wanadaiwa kutishia kumuua mlalamikaji kwa kutumia mkasi ili kujipatia vitu hivyo kwa urahisi.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 22, 2018.