In Summary

Watu wengi wanakula kitimoto lakini ukweli uliopo ni kwamba maeneo mengi hayana machinjio ya nguruwe. Sio machinjio pekee, hata maeneo yam nada kwa ajili ya mifugo hiyo hayapo pia. ndio kwanza mchakato unafanywa ili kutenga maeneo hayo.

Nyama ya nguruwe, ambayo inajulikana zaidi kama “kiti motó” inaliwa na kupendwa na watu wengi, lakini wanaweza kuwa hawajawahi kujiuliza machinjio ya wanyama hao yako wapi.

Si machinjio tu, nguruwe hawaonekani kwenye minada ya kawaida ya mifugo. Huuzwa wapi?

Kwa watu wanaoishi nje ya miji, hasa vijijini, ni rahisi kuona sehemu ambayo wanyama hao wanachinjwa, lakini si mjini ambako imani za kidini hufanya wachinjaji wawe sehemu ambazo hazikwazi wengine. Lakini kutokana na matumizi makubwa ya nyama hiyo, swali linabakia kuwa machinjio yake yako wapi; mnada uko wapi na kama madaktari hupita kupima ubora wa nyama kabla ya kusambazwa kwa walaji.

Hali kadhalika, kujua hali ya usafi ya machinjio hayo kama ambavyo viongozi wa Serikali wamekuwa wakipita katika machinjio ya mifugo mingine kuhakikisha usafi unazingatiwa.

Labda pa kuanzia ni wapi unaweza kukuta mnada wa nguruwe.

Ikitokea una nguruwe 49 na unataka kuwauza wote kwa mkupuo, utaenda wapi ambako unaweza kukutana na wateja wakanunue mzigo wote? Au kama umepata tetesi kuwa sehemu fulani wanahitaji nguruwe wengi, utaenda wapi uweze kuwapata kwa wepesi?

Majibu ya maswali haya ni tofauti kulingana na mahali alipo msomaji kwa sasa kwa kuwa ipo mikoa inayofuga nguruwe wengi na mingine wachache.

Ukweli ni kwamba hadi sasa hakuna sehemu maalumu inayotumika kama mnada wa wanyama hao. Soko la nguruwe ni mawasiliano binafsi ya mnunuzi na muuzaji au mhitaji kufanya utafiti wake kujua mfugaji gani anaweza kuwa na idadi kubwa ya nguruwe.

Kwa mujibu wa ripoti ya mifugo ya Wizara ya Mifugo ya mwaka 2013, idadi ya nguruwe ilikuwa milioni 2.1 na upatikanaji wa nyama ukiwa tani 81,311 kwa mwaka, kiwango ambacho kiliongezeka mpaka tani 648,810 mwaka 2016/17.

Idadi hiyo ni kubwa na ambayo inaonyesha kuna haja ya kuwa na mnada wa uhakika na machinjio ya kisasa kuwahakikishia walaji usalama wa afya zao.

“Serikali inatambua kuwa hakuna machinjio wala maeneo ya mnada kwa ajili ya nguruwe,” anasema Dk John Kaijage, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za mifugo wa Wizara ya Mifugo.

“Serikali inatenga maeneo maalumu ambako mifugo hiyo itauzwa kwa njia ya mnada. Utaratibu unaandaliwa.

“Ni jukumu langu hilo. Ninaandaa mkakati wa kubainisha marketing areas (maeneo ya kunadishia) pamoja na ujenzi wa machinjio ya kisasa yatakayoongeza tija kwa wafugaji na wafanyabiashara.”

Anasema mkakati huo ni maalumu kwa ajili ya mifugo yote ambayo haijapewa kipaumbele, lakini ina mchango mkubwa kwa jamii.

“Misri kuna machinjio ya kisasa na minada ya uhakika (ya nguruwe) inayowakutanisha wafugaji na wafanyabiashara,” anasema Dk kaijage.

“Ingawa ni nchi ya Kiislamu, kila siku nguruwe wengi huchinjwa na kusafirishwa kwenda jijini London, Uingereza. Ni biashara kubwa.”

Kuhusu usalama wa afya, Dk Kaijage anasema pamoja na kutokuwepo na m,achinjio ya uhakika na ya kisasa, nyama ya nguruwe hukaguliwa na maofisa wa afya hasa kwenye mikoa ya nyanda za juu ambako ufugaji wa wanyama hao ni mkubwa. Nyanda za Juu Kusini inaundwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma.

Licha ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Kaijage anasema maeneo mengine yenye nguruwe wengi ingawa wanafugwa kienyeji ni Manyara, Morogoro na Dar es Salaam.

“Kutokana na kukosa machinjio yapo maeneo ambayo nyama ya nguruwe hukaguliwa na ambayo hayana ukaguzi. Mikoa inayofuga zaidi ndiko kuna wataalamu wanaokagua kwenye slaughter slabs (machinjio) yanayoendeshwa na halmashauri au watu binafsi,” anasema Dk Kaijage.

Kabla ya Serikali kutekeleza azima yake ya kujenga machinjio ya kisasa, kwa sasa wauzaji wa nyama hiyo hufanya shughuli hiyo kwa utaratibu tofauti.

Mtaa wa Makoka uliopo maeneo ya Mbagala Sabasaba una moja ya machinjio hayo binafsi.

Machinjio hayo hayatofautiani sana na mengine ya mifugo ya kawaida vile ng’ombe, mbuzi au kondoo. Kuna mabanda mawili makubwa, nje kukiwa na mapipa mawili yaliyo juu ya mafiga. Mapipa yote mawili yamechafuka kwa masizi ya moshi.

Muda wote mapipa hayo hujaa maji ya moto yanayochemka.

“Tunayanatumia kwa ajili ya kunyonyolea kitimoto baada ya kuchinjwa ila ikifika jioni (kuanzia saa 11:00) huwa hayana kazi,” anasema mfanyakazi wa machinjio hayo aliyejitambulisha kwa jina moja la Issa.

Kwa kawaida, nguruwe huwa hachunwi ngozi, bali hunyonyolewa manyoya kwa kutumia kwa kitu chenye makali kama kisu au wembe baada ya kumwagiwa maji ya moto.

Katika moja ya mabanda hayo, kuna nguruwe kama 50 hivi ambao kwa mujibu wa Issa, wote wanamilikiwa na mtu mmoja.

Banda jingine lina vyumba viwili na kimoja kati ya hivyo ndio machinjio. Kimetengenezwa kwa marumaru nyeupe ukutani na sakafu imetapakaa damu.

Juu kuna vyuma viwili vinavyoning’inia kwa ajili ya kuning’iniza nyama ya nguruwe. Pia kuna meza iliyojengwa kwa saruji kwa ajili ya kuwekea nyama.

“Ufanyaji kazi wetu hauna tofauti na machinjio mengine, utaratibu wote hufuatwa,” anasema Issa.