In Summary

Askofu mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF) Zakary Kakobe amemweleza Rais John Magufuli kuwa kazi anazozifanya zinastahili pongezi na hawezi kuwafurahisha wote


Dar es Salaam. Askofu mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF), Zakary Kakobe amemwambia Rais John Magufuli kuwa hata kama atafanya mema kiasi gani hawezi kusifiwa na watu wote na badala yake wengine watatoa sifa hizo siku akifa.

Askofu Kakobe ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 11, 2019 wakati wa kupokea ndege ya pili aina ya Airbus 220-300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Kiongozi huyo wa kiroho amemweleza Rais Magufuli kuwa hata akitoa chakula katika kila kaya nchi nzima, wapo baadhi ya watu watasema anawapelekea sumu.

“Mheshimiwa Rais mimi huwa ni mbishi kidogo na ukiniona nimekanyaga mahali kama hapa ujue umenikosha na sijui kama kuna watu wengine wamekoshwa kama Kakobe kwa ajili ya haya yanayotendeka,” amesema Askofu Kakobe huku akishangiliwa na umati wa watu waliojitokeza

“Na wengine wanasema mnamwabudu na kumsifu wakati hata Biblia inasema anayestahili heshima apewe heshima, hivyo unastahili zote.”

Askofu Kakobe amesema suala la kuwakusanya watu wote bila kujali itikadi huo ndio uzalendo unaotakiwa.

Amesema, “Ukiona hizi shangwe na vigelegele japo sio wote wanaokusifu ujue kuna watu wanashangilia kazi zako na leo tunakusihi ujipongeze, ulale na ujue wapo watu wanakushangilia kwa kazi zako.”