In Summary
  • Wafanyabiashara Uganda wamejikuta katika hali ya furaha baada ya Serikali ya Tanzania kukubaliana na ile ya Uganda katika masuala ya kibiashara, na sasa watakuwa na uwezo wa kuingiza bidhaa zao zikiwemo sukari, alizeti na soya.

Kampala, Uganda. Serikali ya Uganda imesema wafanyabiashara wa nchi hiyo sasa wamepata soko la bure la sukari, alizeti na soya, baada ya makubaliano kati ya nchi hizo mbili kufanyika huko Mutukula, mpakani mwa Uganda na Tanzania leo.

Hayo yamewekwa wazi na wizara ya biashara ya nchini Uganda ikionyesha kuwa bidhaa hizo zimeruhusiwa kuingia Tanzania.

Nchi ya Tanzania miezi kadhaa iliyopita ilizuia uingizwaji wa baadhi ya bidhaa kutoka Uganda, jambo lililosababisha wafanyabiashara kuandamana nchini humo.

Hata hivyo, kutokana na vikao kadhaa, Serikali ya Tanzania imekubali kutoa vibali vya uingizwaji wa bidhaa hizo kwa wafanyabiashara wa Uganda.

Serikali ya Tanzania iliweka masharti hayo ya kuzuia wafanyabiashara kutoka Uganda kuingiza bidhaa hizo kutokana na kutuhumiwa kuingiza sukari toka nje, kisha kuzifungasha upya na kuzisafirisha tena kwenye masoko ya nje.

Uhakiki wa pamoja umefanyika hivi karibuni, kwa ajili ya kupata uhakika wa chanzo cha alizeti na soya, ambapo imethibitika kuwa bidhaa hizo zinakidhi sheria za Shirikisho la Afrika Mashariki katika uasili wake, hivyo kukidhi viwango vinavyohitajika kwa ajili ya mahitaji ya soko hilo la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, uhakiki huo umegundua kwamba mafuta ya nazi kwa ajili ya kupikia vyakula, hayakidhi viwango vya sheria za uasili za Shirikisho la Afrika Mashariki.

Mkutano huo muhimu uliomhusisha Waziri wa  Biashara wa Uganda, Amelia Kyambadde na mwenzake wa Tanzania, Joseph Kakunda, ambao umefanyika Mutukula, mpakani mwa nchi hizo mbili, pia umejadili kuondoa vikwazo vya ushuru na kuhamasisha biashara baina yao.

Pia mawaziri hao ambao walikuwa pamoja na makatibu wakuu wa kudumu katika wizara za biashara kwa nchi zote mbili, wamejadili baadhi ya mambo ikiwemo uwepo wa soko la sukari kutoka Uganda, gharama za watumiaji wa barabara kwa malori yanayotoka Uganda kuingia Tanzania na kibali cha biashara kwa wafanyabiashara wa Uganda wanapoingia Tanzania ambacho kinagharimu Dola za Kimarekani 100.