In Summary

Klabu ya PSG ya Ufaransa imeamua kulishitaki Shirikisho la soka barani Ulaya (Uefa) kwenye mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS), kupinga uchunguzi unaoendelea juu ya usajili wa mastaa wake wawili Neymar na Kylian Mbappe.


Paris, Ufaransa. Klabu ya Paris St-Germain imeamua kuliburuza Shirikisho la soka barani Ulaya (Uefa) kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS).

PSG imefikia uamuzi huo baada ya kamati ya uchunguzi wa masuala ya usajili kudai klabu hiyo ilivunja sheria za usajili kwa wachezaji wake Neymar na Kylian Mbappe.

Timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu Ufaransa baada ya kushinda mechi zote 12 za msimu huu, imepinga uamuzi wa Uefa kuanzisha uchunguzi dhidi yake kuhusu suala la usajili huo.

Uefa kupitia kamati yake ya Haki sawa kwa usajili (FFP) imeanzisha uchunguzi huo baada ya kudai  kuna matumizi mabaya ya fedha yamefanyika katika usajili wa nyota hao.

PSG ilimsajili Neymar Agosti mwaka jana kutoka Barcelona kwa ada iliyoweka rekodi ya Dunia ya Euro 222 milioni sawa na Pauni 200 milioni.

Kama hiyo haitoshi kiangazi cha mwaka huu PSG imefungua pochi na kutoa Euro 180 milioni sawa na Pauni 165.7 milioni kumsajili Mbappe, aliyekuwa akicheza katika timu hiyo kwa mkopo kutoka Monaco.

Mwaka 2014, PSG iliadhibiwa na kamati hiyo ya FFP, kwa madai ya kutumia fedha nyingi katika usajili ingawa utetezi wake ulikuwa kwamba imepata fedha nyingi kutoka kwa wadhamini wake mamlaka ya Utalii kutoka nchini Qatar.

Klabu hiyo ilifungiwa kusajili kwa muda mwaka 2011 na ikalazimika kuwatumia wachezaji 21 pekee katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo lililoifanya itolewe mapema na sasa inaona kama vile inafanyiwa hujuma.

PSG imedai kuwa imewajili nyota hao ili waisaidie kutwaa ubingwa wa Ulaya lakini pia uwepo wao utaongeza thamani ya klabu hivyo sio sahihi kusema wachezaji hao watasababisha klabu hiyo kupata hasara.