In Summary

Kwa wale wasiokuwa na matokeo ni kwamba, usiku wa Jana, Monaco ya Thiery Henry, ilitandikwa 0-4 na Club Brugge, Atletico Madrid 2-0 Dortmund, Barcelona 1-1 Inter,  Tottenham 2-1 PSV, FK Crvena Zvezda 2-1Liverpool, Napoli 1-1PSG, FC Porto 4-1 Lokomotiv Moscow na Schalke 2-0 Galatasaray.


MICHUANO ya ligi ya Mabingwa ulaya inaendelea tena leo. Baada ya jana usiku kushuhudia miamba kadhaa ya soka ikitandikwa bila huruma, leo macho na masikio, yanaelekezwa katika viwanja nane tofauti barani Ulaya.

Kwa wale wasiokuwa na matokeo ni kwamba, usiku wa Jana, Monaco ya Thiery Henry, ilitandikwa 0-4 na Club Brugge, Atletico Madrid ikaitandika Borrusia Dortmund 2-0, Barcelona na Inter zikatoka sare ya 1-1.

Tottenham Hotspur, ikailaza PSV Eindhoven 2-1, Liverpool ikalimwa 1-2 na FK Crvena Zvezda, Napoli na PSG zikatoshana nguvu (1-1), FC Porto ikaitandika Lokomotiv Moscow 4-1 huku Schalke 04 wakiilamba Galatasaray 2-0.

Leo Usiku, FC Bayern Munchen itaumana na AEK Athens, Benfica v Ajax, Lyon v Hoffenheim, Manchester City wakiikaribisha Shakhtar Donetsk pale Etihad, CSKA Moscow v Roma, Viktoria Plzen v Real Madrid, Valencia v Young Boys na Juventus itailika Manchester United, nchini Italia.

Kuelekea mechi hizo sasa, Mwanaspoti Digital, inakuchambulia hatua kwa hatua mechi zote hizo kuanzia mechi ya Juventus dhidi ya Mashetani wekundu hadi ile ya Bavarians dhidi ya AEK Athens, katika number.

Juventus v Manchester United

5 - Cristiano Ronaldo, ameshindwa kupata bao hata moja katika mechi tano za hivi karibuni za ligi ya mabingwa Ulaya. Mara ya mwisho kufunga bao kwenye UEFA, ilikuwa Aprili, akiwa na Real Madrid, akiifunga klabu yake ya sasa (Juventus).

2 - Sambamba na Bayern Munich, Manchester United, ni moja ya timu mbili pekee, zilizowahi kushinda mechi za ugenini mara mbili, dhidi ya Juventus.

Benfica v Ajax

5 – Ajax hawajapoteza mchezo hata mmoja katika mechi tano za hivi karibuni walizocheza dhidi ya Benfica. Wanarekodi ya kutoa sare moja na kushinda michezo minne. Mechi ya mwisho kukutana walishinda 1-0. Mechi hii ilipigwa, Oktoba mwka huu, katika uwanja wa Cruijff Arena.

4 – Benfica wameambilia alama nne tu katika michezo 11 za ligi ya mabingwa Ulaya, hatua ya makundi. Wamepoteza mechi nne za mwisho walizocheza katika uwanja wa nyumbani.

Lyon v Hoffenheim

6 - Lyon wamekuwa wabishi msimu huu kwenye Uefa, kuliko walivyokuwa miaka 10 iliyopita. Katika mechi sita walizocheza mpaka, hawajapoteza hata moja. Mara ya mwisho kuandikisha rekodi kama hii ilikuwa kati ya Septemba 2006 na Februari 2007.

5 – Kwa Upande wao, Hoffenheim wanapata tabu sana. hawajashinda mechi hata moja katika mechi tano za mwisho za ugeni za Uefa. Wana rekodi ya sare mbili na vichapo vitatu.

Manchester City v Shakhtar Donetsk

4 – Kama watafungwa leo usiku, City wataweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya EPL, kupoteza mechi nne mfululizo katika uwanja wa nyumbani, kwenye michuano ya Uefa/Uropa.

24 – City walifanikiwa kupiga mashuti 24 yaliyolega goli, katika ushindi wa 3-0 walioupata dhidi ya Shakhtar, walipokutana kwa mara ya mwisho. hii iliwafanya City kuwa klabu ya pili, iliyotia fora kuwanyanyasa Shakhtar baada ya Real Madrid (26).

CSKA Moscow v Roma

23 – Wastani wa umri wa wachezaji waliounda kikosi cha kwanza CSKA Moscow, walipotandikwa 3-0 mjini Roma, ilikuwa miaka 23 na siku 92. Hii ilikuwa mwezi Oktoba. Hiki kilikuwa kikosi changa zaidi kuwahi kucheza Uefa, baada ya miaka minne. Novemba 2014, wastani wa wachezaji wa mechi ya Ajax v PSG, ilikuwa miaka 22 na siku 305.

10 - Edin Dzeko ndio kinara wa kufania nyavu kwenye msimu huu wa Uefa. Mpaka sasa ameshaweka mabao 10 kambani. Wanaofuatia wamefunga chini ya mabao nane.

Viktoria Plzen v Real Madrid

9 – Katika mechi tisa zilizokutanisha klabu kutoka Czech na klabu ya Hispania kwenye ligi ya mabingwa, klabu za La Liga, ziliibuka kidedea, wakifunga zaidi ya mabao mawili.

8 - Gareth Bale yupo katika kiwango kizuri na amehusika katika upatikanaji wa mabao nane, katika mechi saba za Uefa, alizocheza na jezi ya Los Blancos, msimu huu. (mabao manne na Asisti nne).

Valencia v Young Boys

6 – Baada ya kufungwa mara nne na kutoa sare mara mbili, katika michezo sita za hivi karibuni za Uefa, Valencia wamejikuta katika rekodi mbaya ya kukosa ushindi kwenye michuano hiyo na kurudia kile kilichowatokea, mwezi Oktoba 2011.

42  -Valencia na Younga Boys, wameandikisha mashuti 42 kila mmoja, katika msimu huu tu wa Uefa, huku wakifunga mara moja kila mmoja kutokana na mashuti hayo. Hatari!

Bayern Munich v AEK Athens

10 – Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich ni wababe wa wagiriki. Hawajapoteza mchezo hata mmoja katika mechi 10, zilizowakutanisha na klabu kutoka Ugiriki.

18 – Bavarians wamefumania nyavu za wagiriki mara 18 bila jawabu katika mechi tano za hivi karibuni. Je, AEK Athens wataweza kutafuna mfupa huu uliowashinda ndugu zao?

23 – AEK wanapambana kufuta gundu ya kukosa ushindi katika michezo 23, kwenye michuano ya Uefa na kombe la Uropa. Je watafanikiwa mbele ya Bavarians? Yetu macho na masikio.