Pengine ndiye mwanasiasa aliyemaliza mwaka uliopita akiwa staa zaidi na ndiye mwanasiasa aliyeuanza mwaka akiwa staa zaidi. Aggrey Mwanri, mkuu wa mkoa wa Tabora. Ni staa sana na anaburudisha.

Baada ya Watanzania kuchoshwa na maisha au maongezi magumu, wameamua kumfanya Mwanri kuwa staa. Kila kukicha video zake zinasambaa huku na kule katika mitandao ya kijamii. Wanaipenda sura yake na wanaipenda mikwara yake. ‘injiniaaa soma hiyoo’.

Wasanii mastaa wanaposti video zake mitandaoni. Wanamichezo wanafanya hivyo hivyo. Watu wengine maarufu wanafanya hivyo hivyo. Na sasa upo mchezo wa kukata vipande vya video zake na kuunganisha na matukio mengine.

Anapokuja Dar es Salaam akitoka Tabora, Mwanri huwa anapokewa na vituo vya redio na televisheni kwa ajili ya mahojiano maalumu. Si kwamba wanamualika atuambie maendeleo ya mkoa wa Tabora, hapana, wanataka tu kuwa karibu naye. Ni staa.

Watanzania wanajua Mwanri hayupo kama anavyotaka aonekane. Walio karibu naye wanajua ni mtu muungwana ambaye anataka kazi zake ziende huku akiweka mikwara ndani yake. Huwa hadhalilishi watu ovyo katika kazi zao. Anachotaka ni kutembeza mikwara tu. Hafukuzi mtu kazi ovyo wala hatukani mtu.

Hata wale ambao hawapo karibu na Mwanri ambao wanamtazama katika video zake tu wanajua kwamba Mwanri si mkali isipokuwa anapenda mikwara. Kama angekuwa mkali wangemuweka kando na wala wasingemfanya kuwa staa. Watanzania hawampendi mtu mgumu ambaye anataka kufanya mambo kuwa magumu kila wakati.

Wakati mwingine Watanzania ni watu wa ajabu. Hauwezi kujua wanachotaka. Ukijifanya unaongea mambo mazito, ukataka kujifanya wewe ni mzalendo sana, ukataka kuwapa takwimu nzito hadharani, usidhani kama watakupenda sana. Wanachoka kukusikiliza na hotuba zinazojirudiarudia. Wanataka mtu ambaye atawaburudisha pia, ndio maana wamemchagua Mwanri.

Kuna nyakati ambazo naamini baadhi ya wanasiasa wanakerwa na umaarufu wa Mwanri. Wasikereke bali wajifunze tu kuwasoma wananchi. Ndio maana Watanzania walimpenda Mwalimu Nyerere na walipenda kumsikiliza katika hotuba zake. Maisha yalikuwa magumu lakini aliwalainisha katika hotuba zake.

Namuomba tu Namba Moja asimtumbue Mwanri. Amuache atupe burudani. Injianiaaa soma hiyooo!