In Summary

Zitto Zuberi Kabwe akihisi kuna watu au mtu wa Kigoma anaonewa  husikika akisema “Jamani Wazee wa Kigoma tukutane kujadili hili”

HUWA ananikosha sana mtoto wa Mzee Zuberi Kabwe, Zitto. achana na weledi wake wa mambo kama mwanasiasa na msomi, havinihusu sana. Ananikosha kwa mikwara yake ya kuonyesha watu wa Kigoma ni watu wa aina gani. kwamba sio wa kuchezewa.

Ana mkwara wake mmoja naupenda sana. Akihisi kuna watu au mtu wa Kigoma anaonewa basi Zitto husikika akisema “Jamani Wazee wa Kigoma tukutane kujadili hili”. Unajua anamaanisha nini? Kwamba Wazee wafanye ‘kazi yao’ kama kuna mtu anaonewa kweli basi aliyesababisha hayo aokote makopo.

Zitto akisema hivyo natabasamu. Nasikia Kigoma sio mchezo. Wakati Bwana mdogo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo alipoanza kuhojiwa kuhusu uraia wake, Zitto akahamaki. Akawataka wazee wa Kigoma wakutane ‘Kujadili hilo’.

Lakini pia huku uswahilini kwetu Zitto akisema kuhusu Wazee wa Kigoma huwa tunamwamini. Unajua kwa nini? Kwa muda mrefu yeye mwenyewe ni mmoja kati ya wanasiasa ambao wanakosoa sana utawala huu lakini hakuguswa.

Tukajua kwamba Zitto anaogopwa kwa ule mkwara wa ‘Wazee wa Kigoma tukutane kujadili hili’. Tetesi za ndani zikasema anaogopwa kweli. Kuna wakati aliwahi kusema ‘Mkitaka kuniteka nyumbani kwangu mtakuta bahari tu’.

Hata hivyo, mapema wiki hii ndipo Zitto amepishana na Abdul Nondo katika vyombo vya sheria. Wakati Nondo akiachiwa huru, saa 72 kabla, Zitto alikuwa akipanda kizimbani kwa kosa ambalo ni wazi litakuwa la uchochezi. Ni ngumu kutenganisha makosa ya wanasiasa wa kileo na uchochezi. Achana na hilo. Tunajiuliza Polisi waliona nini walipokwenda kumkamata Zitto ambaye kwetu sisi wengine ni mara ya kwanza kumuona akipandishwa kizimbani.

Nasubiri kwa hamu kupata stori ya mauzauza waliyoona wakati wanakwenda kumshika kwake Masaki. Lakini pia Zitto ni rafiki yangu, kwa hiyo nitampigia simu kumuuliza kama aliwasamehe au Wazee waliamua tu kuachia aende Kisutu.

Nchi ina raha yake hii bwana. Asikwambie mtu. Kila mtu ana mikwara yake. Mtoto wa Marehemu Mama Shida Salum huwa ananikosha kwa mkwara huo tu. ‘Wazee wa Kigoma tujadili hili.’ Sasa sijui kwa nini kapishana na mdogo wake, Nondo pale Kisutu. Nitarudi na jibu siku nyingine nikishaongea naye.

Soma Zaidi: