Nataka kuanzisha mbio zangu za Marathon. Najua zitaungwa mkono na wengi. Siku hizi mbio za Marathon ni nyingi. Tulia Marathon pale Mbeya, Kilimanjaro Marathon, Tanga Marathon, Morogoro Marathon. Zipo nyingi kwelikweli zinaibuka kama uyoga.

Kisa? Wanasema kuchunga afya zetu. Ni kweli umakini wa kuchunga afya zetu umeanza utawala huu? Sidhani. Tangu somo la Sayansi Kimu zamani, mpaka leo watu tunajua umuhimu wa kuchunga afya zetu. Sawa, magonjwa yanaongezeka lakini ukweli ni kwamba yalikuwepo tangu enzi hizo.

Marathon za nyakati hizi zinakuja kwa sababu tuna muda mwingi wa kuwa makini na familia kuliko kwenda baa. Tuna muda mwingi wa kukimbia barabarani kwa sababu hatusafiri tena, hasa kwa wale rafiki zangu wafanyakazi wa Serikalini ambao kila siku walikuwa wakipishana hewani. Mara London mara Dubai mara Hongkong mara Washington.

Sasa hivi Mtanzania wa kawaida ana muda zaidi jioni inapoingia. Fedha mfukoni haipo. Utakwenda wapi? Ukisikia Marathon unakwenda kujiandikisha, unaanza mazoezi. Unaanza kukimbia kando ya barabara na washkaji. Sababu za kujitetea kwamba Marathon ni muhimu inabakia kuwa afya tu. Nyingine hatuzisemi.

Hapa ndipo tunapomshukuru Mungu kwa kutupa pumzi ya bure kabisa. Laiti kama na pumzi yake tungekuwa tunalipia, kama tunavyolipa bili za baa si ajabu tungebakia majumbani tu. Tusingekwenda baa wala kujiandikisha Marathon.

Tuendelee kufanya mazoezi binafsi kwa lazima. Wakati wa kufanya mazoezi kwa hiyari hatukuutumia sana. Vikao vyetu vingi vya kutengeneza dili vilianzia saa 10 jioni wakati tunatoka kazini. Sasa hivi dili hakuna basi muda huo unakuwa muhimu kwa kufanya maandalizi ya Marathon.

Natabiri kufikia mwaka 2025 mikoa yote ya Tanzania itakuwa na mbio za Marathon. Baada ya hapo tutaangalia upepo wa utawala mwingine utakavyokuwa. Kama utatulazimisha tuendelee na Marathon basi sawa, kama utakuja utawala mwingine kama ule wa awamu ya nne nadhani kuanzia saa 10 jioni tutarudi katika vikao vya dili tena. Sio maandalizi ya Marathon.