In Summary

Wajasiriamali wabunifu kupata mitaji na mafunzo ya kukuza biashara zao kupitia shindano la biashara ndogondogo lijulikanalo kama "Startupper of the Year" kwa kushindanisha miradi itakayochangia mabadiliko chanya kwenye jamii.


Dar es Salaam. Wajasiriamali wabunifu nchini watapata fursa ya kupata mitaji pamoja na mafunzo maalumu kwa ajili ya uendeshaji wa biashara nchini kupitia shindano liitwalo "Startupper of the year Challenge".

Shindano hilo la pili kufanyika nchini linaloendeshwa na Kampuni ya Mafuta ya Total Tanzania, limewalenga vijana wenye mawazo ya biashara na miradi inayoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zao.

Akizungumza leo Oktoba 10, 2018 wakati wa uzinduzi wa shindano hilo, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya Total, Thomas Biyong amesema mbali na Tanzania shindano hilo litafanyika katika nchi 40 barani Afrika ikiwa ni mpango wa kuinua kazi za ubunifu.

"Miradi itapimwa kulingana na wazo la ubunifu wa asili, umuhimu kwa jamii pamoja na uwezekano wa mradi kuwa endelevu," amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Mahusiano wa kampuni hiyo, Masha Kileo amesema wabunifu watakaoshiriki wanatakiwa kuwa na biashara isiyozidi miaka miwili au chini pamoja na wale wenye mawazo mapya.

"Washiriki watapata mafunzo maalumu juu ya uendeshaji, uangalizi pamoja na namna ya kuboresha biashara zao," amesema.

Mshindi atapata Sh30 milioni, wa pili Sh20 milioni na wa tatu Sh15 milioni kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi watakayoibuni hapa nchini.

Shindano la kwanza lilifanyika mwaka 2015 ambapo Iddi Kalembo wa Mtwara aliibuka mshindi kwa mradi wake wa upigaji picha kwa njia ya simu hasa vijijini.