In Summary
  • Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache zinazotoa usafiri huo kwa njia rasmi.

Dar es Salaam.Wakati Serikali ikipendekeza kuwa na pikipiki zinazobeba abiria wengi, Kampuni ya Taxify imezindua huduma ya usafiri wa bodaboda jijini Dar es Salaam na Mwanza kwa ajili ya wasafiri wenye haraka wanaoshindwa kuwahi waendako kutokana na foleni ya magari.

Kwa kutumia App ya Taxify inayopatikana kwenye simu za kisasa za mkononi, Watanzania wanaweza kupata usafiri wa bodaboda kwa urahisi na bei nafuu na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu ambayo huduma hiyo imezinduliwa. Huduma hiyo inapatikana pia Kenya na Uganda.

Meneja mkuu wa Taxify Afrika Mashariki, Shivachi Muleji amesema kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Estonia ilibuni huduma ya bodaboda kutokana na kuongezeko kwa uhitaji wa usafiri huo ambao ni usalama na wa uhakika.

"Tatizo la foleni limechochea uhitaji wa usafiri wa pikipiki katika Jiji la Dar es Salaam. Usafiri wa usalama na uhakika ni kipaumbele kwa wasafari wengi. Huduma yetu inatoa suluhisho kwa changamoto hizi,” amesema leo, Septemba 8, 2018.

Meneja mkuu wa kampuni hiyo nchini, Remmy Eseka amesema huduma ya Taxify boda imejikita kuhakikisha usalama wa madereva na abiria.

Amesema teknolojia yao inawawezesha kufuatilia tabia ya madereva na kumpa abiria uwezo wa kutoa maoni kuhusu huduma za dereva na safari yake kila anapotumia huduma hiyo.

“Kampuni imeweka mwongozo utakaohakikisha usalama wa abiria na madereva, wote watahitajika kuvaa kofia ngumu na reflector (jaketi linaloakisi mwanga). Mteja hatoruhusiwa kukaa upande isipokuwa kwawalemavu,” amesema Eseka.