In Summary
  • Waziri Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa TB unatibika na inawezekana kupambana nao ikiwa kila mtu atashiriki kwa nafasi yake

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanzisha ushirika wa wadau wa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu 'Stop TB Partinaship' baada ya takwimu kuonyesha kuna changamoto zinazokwamisha mapambano hayo.

Takwimu zinaonyesha kila mwaka kunazalishwa wagonjwa 154,000 huku kifua kikuu sugu kikizalisha wagonjwa 443.

Akifungua mkutano wa kwanza wa ushirika huo leo Jumatatu Aprili 15,2019 Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu amesema zinahitajika juhudi za pamoja kupambana na kifua kikuu.

Ummy amesema mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hajapata matibabu anaweza kuambukiza watu 10 mpaka 20 kwa mwaka.

"Kila mtu anatakiwa kupambana na ugonjwa huu ili kudhibiti, sijawaona waganga wa jadi hapa lakini tafiti iliyowahi kufanywa inaonyesha ni waathirika kwa sababu wanaishi na wagonjwa," amesema Ummy.

Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuingia kwenye ushiriki huo ili wasaidie kutoa elimu kwa waumini wao kwa kuweka suala la kifua kikuu kwenye mahubiri yao.

"Mkakati ni kuwafikia, kuwaibua na kuwaweka kwenye matibabu wagonjwa kwa sababu ugonjwa huu unatibika," amesisitiza.

Awali, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Bakari alisema Tanzania ni kati ya nchi 30 zinazosemekana kuwa na wagonjwa wengi wa TB.

Profesa Bakari amesema Serikali imeweka juhudi katika kupambana na ugonjwa na miongoni mwake ni kuundwa kwa ushirika huo utakaofanya kila mtu kushiriki.