In Summary

Hayo yameelezwa leo Juni 14  na Naibu waziri wa afya Dk Faustine Ndugulile wakati wa kilele cha Wiki ya Mafamasia iliyofanyika Mnazi Mmoja, jijini hapa.

Dar es Salaam. Serikali imesema  usugu wa dawa unasababishwa na tabia ya baadhi ya mafamasia, kugawa dawa bila kufuata kanuni na taratibu za taaluma hiyo.

Hayo yameelezwa leo Juni 14  na Naibu waziri wa afya Dk Faustine Ndugulile wakati wa kilele cha Wiki ya Mafamasia iliyofanyika Mnazi Mmoja, jijini hapa.

Dk Ndugulile amesema kuwa famasia wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria ikiwamo kuepuka kugawa dawa kwa wagonjwa bila kupata ushauri wa daktari.

Amesema changamoto hiyo inatokana na famasia kutoa dawa kiholela bila kuwapima wagonjwa na kujikuta wanasababisha usugu wa dawa kwa sababu wagonjwa wanapewa zisizo sahihi kwa maradhi yao.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, Dk Ndugulile amesema kuwa kwa sasa hali ni nzuri na zinapatikana kwa asilimia 91.

“Sitegemei kama kuna mwananchi atakwenda kutibiwa na kupewa cheti akanunue dawa nje, dawa zinapatikana na nimetembelea mikoa mingi nimeona hali ni nzuri, ”amesema Dk Ndugulile.

Kuhusu watengenezaji dawa wa ndani Dk Ndugulile amesema kuwa serikali inaunga mkono sekta binafsi ya dawa.

Amesema kutokana na hilo atakutana nao pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) kuangalia namna ambavyo watatoa nafasi ya kwanza ya kununua dawa zao kwa sababu imeonekana ni changamoto.

“Nimetembelea mabanda nimekutana na watengeneza dawa, kwa kweli wanajitahidi dawa ni nzuri na zina ubora, ingawa MSD haifanyi nao kazi ipasavyo.