In Summary
  • Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu leo Jumanne, ametembelea Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) na kushauri kubumi mbinu ya kutangaza utalii wa ndani kwa kutumia watu mbalimbali

Dar es Salaam. Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) imetakiwa kuweka mikakati ikiwa ni pamoja na kuwatumia wanataaluma kutangaza utalii wa ndani.

Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Januari 8, 2019 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu alipotembelea bodi hiyo.

Kanyasu amesema hazijafanyika juhudi za kutosha za kuwafikia watu wanaoweza kuutangaza utalii wa ndani.

“Mnaweza kukutana na wakuu wa vyuo mkafanya kutembelea hivi vivutio kuwa ni sehemu ya masomo ya wanafunzi, hii itasaidia hata wao wanafunzi kuwa wabunifu kwa kutangaza vivutio na kuibua fursa nyingine nyingi ambazo pia zitachangamsha utalii wa ndani,” amesema.

Kanyasu ambaye pia ni mbunge wa Geita Mjini (CCM) amesisitiza matumizi ya teknolojia katika kutangaza vivutio vilivyopo huku akiesema bodi hiyo inapaswa kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

“Msijibane watumieni mabalozi wa hiyari walioko nje ya nchi watusaidie kutangaza, mfano tukipata bloger maarufu pale New York (Marekani) akawa ana tweet angalau mara moja kwa wiki kuhusu vivutio vyetu watu wengi watakuja,” amesema.

Pia, Kanyasu ameshauri kuwapo utaratibu wa kuwaalika wana michezo wa kimataifa yanapofanyika mashindano mbalimbali ikiwemo riadha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Devotha Mdachi amesema ipo mikakati kadhaa ambayo wamejiwekea kwa mwaka huu kuhakikisha wanatekeleza jukumu la kutangaza vivutio.

Amesema bodi hiyo ipo kwenye mazungumzo na mchezaji wa Tanzania anayecheza soko la kulipwa Ubelgiji katika timu ya KRC Genk, Mbwana Samatta kwa ajili ya kuwa balozi wa utalii nchini humo.

Pamoja na huyo wengine wanaofikiriwa ni Yussuf Poulsen anayechezea timu ya Taifa ya Denmark ambaye ana asili ya Tanzania pamoja na mwanamitindo Flaviana Matata.