In Summary
  • TRA imetangaza msamaha huo baada ya mkutano kati ya Rais John Magufuli na Baraza la Wafanyabiashara uliofanyika Machi 20, 2018.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza msamaha wa riba na adhabu ya madeni ya kodi kwa wafanyabiashara.

TRA imetangaza msamaha huo baada ya mkutano kati ya Rais John Magufuli na Baraza la Wafanyabiashara uliofanyika Machi 20, 2018.

Taarifa iliyotolewa na TRA leo Julai 11, imesema msamaha huo umetokana na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu.

“Bunge la Jamhuri ya Muungano limefanya marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na sehemu ya sheria ya Usimamizi wa Kosi ya mwaka 2015,” imesema taarifa hiyo.

Imeongeza: “Katika marekebisho hayo Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kutoa msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ya awali.”

Lengo la msamaha huo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kutoa unafuu kwa walipa kodi wenye malimbikizo ya riba ya na adhabu ili walipe madeni ya msingi ya kodi kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19 na kuwapa motisha ya kulipa kwa kodi kwa hiyari na kwa wakati.

Taarifa hiyo imetaja kodi zitakazohusika na msamaha huo kuwa ni zile zinazotozwa kwa mujibu wa sheria ya TRA, isipokuwa ushuru wa forodha unaosimamiwa na Sheria ya ushuru wa forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.