Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), linajipanga kutekeleza mradi kabambe wa kusambaza gesi asilia kwenye makazi ya watu utakaofuta matumizi ya mkaa kwa ajili ya kupikia.

Mpango huo unakuja wakati Tanzania ikipoteza hadi hekta 400,000 za miti kwa mwaka kutoka na uchomaji wa mkaa, kuni na matumizi mengine.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Misitu (Naforma) ya mwaka 2015, Tanzania ina eneo la hekta 48.2 milioni za misitu ikiwa ni sawa na asilimia 54.6 ya ardhi yote.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri wa misitu ikiwa na mita za ujazo 3.3 bilioni za miti ya asili ambayo ni asilimia 97 ukiondoa miti ya kupandwa.

Hekta 27 milioni za miti hiyo ziko kwenye maeneo ya hifadhi kama mbuga za wanyama, vyanzo vya maji na hivyo hairuhusiwi kisheria kuvunwa miti yake.

Tanzania inategemea misitu kwa asilimia 90 ili kupata nishati ikiwa ni pamoja na kuni, mkaa na mabaki ya mazao ya miti.

Petroli inategemewa kwa nishati kwa asilimia 8 huku umeme ukitoa nishati kwa asilimia mbili.

Ni katika juhudi hizo za kutafuta nishati mbadala itakayopunguza matumizi ya miti kupata nishati, TPDC imeanza kusambaza gesi asilia kwenye makazi ya watu ili waachane na matumizi ya mkaa pamoja na kuni.

Mradi mkubwa wa gesi asilia

Kaimu mkurugenzi wa Mkondo wa Chini wa TPDC, Emmanuel Gilbert anasema usambazaji wa gesi unaendelea na utatekelezwa kwenye maeneo ya Mikocheni, Mlalakua na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini humo, kutokana na bajeti ya shirika ilivyo.

Anataja mradi mkubwa wa kusambaza gesi unaotarajiwa kutumia Dola 270 milioni (sawa na zaidi ya Sh623.97 bilioni) utakaosambaza gesi kwenye makazi kwa mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara ukihusisha sekta binafsi.

“Tunao mradi wa kusambaza gesi utakaohusisha sekta binafsi (PPP). Yaani kampuni binafsi zitakazoshinda tenda ndizo zitakazojenga miundombinu kwenye hiyo mikoa na kununua gesi ya kusambazia wananchi,” anasema Gilbert.

Anasema kwa mkoa wa Dar es Salaam wanatarajia kuwa na kampuni tatu ambapo moja itafanya wilayani Ilala nyingine itakuwa Kinondoni na Ubungo, na kampuni ya tatu itashika wilaya za Temeke na Kigamboni.

Anaongeza kuwa baada ya ujenzi na miundombinu uuzaji wa gesi hiyo utadhibitiwa na Wakala wa Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ili wasiwaumize wateja wao.

Kuhusu muda wa utekelezaji wa mradi huo, Gilbert anasema hadi Mei 2020 mchakato wa zabuni utakuwa umekamilika na kampuni zitakuwa zimeanza kazi.

“Sisi kama Serikali tutaweka vigezo vyetu kwa kampuni na tutakuwa tunafuatilia kila mwaka kujua kama kampuni imetekeleza makubaliano ya kuunganisha wateja. Mikataba yenyewe ni mirefu kati ya miaka 20 hadi 25.”

Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia ambapo kiasi kilichogundulika mpaka sasa ni futi za ujazo trilioni 57.54 (kabla ya kuhakikiwa kiasi kamili kinachoweza kuvunwa).

Kati ya hizo, futi za ujazo trilioni 47.08 ni kutoka vitalu vya kina kirefu cha bahari na futi za ujazo trilioni 8 ni kutoka vitalu vya nchi kavu.

Gesi hiyo inayovunwa hutumika kuzalisha umeme na matumizi ya nyumbani.

Kwa sasa mteja mkubwa wa gesi hiyo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo linaitegemea kwa asilimia 50 kuzalishia nishati hiyo na uwekezaji bado unaendelea.

Gesi pia hutumika viwandani ambapo hivi sasa kuna viwanda 42 vilivyounganishwa na mabomba.

Vilevile, mpaka sasa TPDC imeshaunganisha nyumba 74 na mabomba ya gesi na bado uunganishaji unaendelea.

Mbali ya hayo, kuna kituo cha kujaza gesi magari kilichopo Ubungo, Dar es Salaam ambapo zaidi ya magari 100 yameshabadilishwa na kuwekewa mitambo ya kutumia gesi hiyo badala ya mafuta.

Wateja wafurahia gharama Miongoni mwa watu wanaofurahia matumizi ya gesi ni mama wa nyumbani, Angela Joseph wa Mikocheni jijini Dar es Salaam ambaye anasema tangu ameanza kuitumia amepata unafuu mkubwa kutokana na gharama alizokuwa akizitumia awali kununua mkaa na mafuta.

“Kabla ya kuanza kutumia gesi hii nilikuwa nanunua mkaa gunia moja kati ya Sh60,000 hadi 80,000 ambalo halikutosha hata kwa (matumizi ya)mwezi mmoja,” anasema Angela.

“Lakini nilipounganishwa na gesi nanunua ya Sh50,000, natumia miezi miwili. Hapo situmii nishati nyingine zozote kupikia, ni gesi tu. Tangu chai asubuhi, chakula mchana na usiku na maji ya kuoga. Kwa hiyo ni nafuu zaidi.”

Raymond Kavishe anayepika katika jiko la gesi katika baa iliyopo Mikocheni, anasema amekuwa akitumia mkaa wa Sh15,000 kwa siku kuandaa chakula cha wateja wake, lakini gesi hiyo imemsaidia kupunguza gharama alizokuwa akitumia kwenye mkaa.

“Nimepunguza gharama mara mbili kwa matumizi ya gesi hii. kabla ya gesi hii nilikuwa natumia hadi mkaa wa Sh15,000 kwa siku, lakini sasa nimepunguza gharama hizo mara mbili,” anasema Kavishe.

Ni bora na isiyo na madhara

Ofisa Utafiti wa TPDC, Eva Swillah anasema matumizi ya gesi hiyo ni salama na nafuu kulinganisha na nishati nyingine.

“Hii ni gesi asilia inayochimbwa kwenye visima ikiwa gesi hivyo hivyo. Ni tofauti na gesi ya petroli (LPG) ambayo huwa katika mfumo wa kimiminika,” anasema Swillah.

Anasema gesi hiyo ni salama kwa kuwa ni nyepesi kuliko hewa, hivyo hata inapotokea upenyo ikavuja, hupeperuka hewani na kuepusha madhara, tofauti na LPG ambayo ikivuja hubaki chini kwani ni nzito kuliko hewa.

Ili kuunganishwa na wateja, Swillah anasema hupunguzwa kwanza msongo wake ili iweze kutumika kwenye majiko.

Kuhusu gharama, anasema kwamba kwa sasa TPDC ndiyo inalipia gharama za kuwaunganisha wateja ili kuwashawishi kujiunga na mfumo huo, lakini baada ya hapo mteja ananunua gesi kupitia kwenye mita aliyofungiwa.

Anasema wamekuwa wakiwafuata wateja na kuwashawishi kuunganishwa na mfumo huo ili kuharakisha uunganishwaji wa gesi.

“Tanzania tunayo gesi ya kutosha kabisa kutumika nchi nzima. Changamoto ni ujenzi wa miundombinu ili kuwafikishia wateja kutegemea bajeti inayopatikana.”