In Summary

Mkurugenzi wa TPB Jema Msuya amesema wametoa kompyuta hizo kwa wakulima kutokana na mahusiano bora waliyonayo na wakulima wa korosho.

Mtwara. Wakati wakulima wa zao la korosho wakielekea katika msimu mpya wa mavuno 2018/19, Benki ya Posta Tanzania (TPB) imetoa kompyuta 15 zenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni kwa  Vyama vya Ushirika (Amcos) ili kuwarahisishia ufanyaji kazi na uhifadhi wa kumbukumbu.

Awali watendaji wa Amcos hizo walikuwa wakitumia makaratasi kuhifadhi kumbukumbu na kutumia kompyuta za watu binafsi kufanyia kazi.

Akizungumza leo Septemba 13 wakati wa kukabidhi kompyuta hizo, Mkurugenzi wa Teknohama na Uendeshaji wa TPB, Jema Msuya kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, amesema kutokana na mahusiano mazuri ya benki na wakulima wa korosho hawakuwa na budi kuwakabidhi kompyuta hizo.

“Kwa mwaka 2017 Mtwara pekee tuliweza kufanya kazi na Amcos 22, tunashukuru tumeweza kutoa mchango wetu katika kuboresha zao la korosho na sasa tunategemea kupata wakulima wengi zaidi,”amesema Msuya.

Mrajisi msaidizi wa mkoa, Salum Issa amesema kutolewa kwa kompyuta hizo ni jambo la muhimu kwani Amcos hizo hufanya kazi na taasisi nyingi za kifedha lakini ni mara ya kwanza kupewa vitendea kazi hivyo.

“Tunaingia katika teknolojia ya kompyuta mfano utayarishaji wa mchanganuo wa malipo, kompyuta hizi zitarahisisha kazi kwa hiyo tunatarajia msimu huu zitaongeza kasi ya malipo kwa wakulima lakini kuhifadhi kumbukumbu na wakulima watahamasika zaidi kujiunga na benki,”amesema Issa.

Katibu wa Makini Amcos, Hamis Uledi amesema kwa sasa wataondokana na changamoto ya utunzaji wa karatasi lakini pia kuondokana ya kukosewa kwa taarifa sahihi za wakulima.

“Siku za nyuma tulikuwa tunapata matatizo makubwa kuchapa kazi zetu kwa watu binafsi kwa sababu kila mtu alikuwa anaangalia namna ya kukuharibia, kwa hiyo baadhi ya makatibu wengine tuliwekwa ndani na hata kuuziwa mali zetu kumbe waliotuharibia ni wale tuliowatumia kuchapa kazi zetu,”amesema Uledi.