In Summary

Lengo ni kusambaza huduma hadi ngazi ya chini ambako kuna wateja wengi

Dar es Salaam. Shirika la Posta Tanzania (TPB) limesema baada ya kufanikiwa kufikisha huduma zake katika ngazi ya wilaya, sasa lipo mbioni kusogea hadi kwenye kata.

 

Hayo yalisemwa leo na Postamasta Mkuu wa shirika hilo, Hassan Mwang'onde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa shirika hilo katika  mkutano wa dharura wa Umoja wa Posta Duniani uliofanyika Istanbul, Uturuki Septemba 3 hadi 7 mwaka huu.

 

Alisema mkutano huo umeliwezesha shirika hilo kujifunza mengi na kuwapa ari ya kuendelea kusambaza huduma hadi ngazi ya chini ambako  kuna wateja wengi.

 

"Tunataka ifike mahali mwananchi aweze  kupata huduma kama ya kitambulisho cha uraia na kupokea vifurushi mbalimbali akiwa ndani ya kata yake na siyo kufunga safari kwenda wilayani jambo ambalo Posta uwezo huo tunao,” alisema.

 

Alisema wakati posta ikiwa na mitandao 600,000 duniani, ni fursa kwa shirika hilo kuongeza ufanisi ili kukidhi hali ya sasa ya soko kwa kutumia mtandao huo wa soko.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi wa shirika hilo, Dk. Haruni Kondo alisema  wamejifunza mambo mengi ikiwamo namna ya kupunguza gharama za kufanya mikutano kwa kutumia teknolojia bila ya kutumia karatasi.