In Summary

Kutokana na changamoto za masoko na ajira Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeandaa Kongamano la wadau wa zao la korosho litakalofanyika mkoani Mtwara Julai 12 na 13, 2019 lengo likiwa ni kuongeza ushindani katika soko, ushawishi wa kuwekeza katika mnyororo wa thamani ya zao hilo ili kuongeza ajira na mapato. 

 


Dar es Salaam. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimeandaa Kongamano la wadau wa korosho litakalofanyika mkoani Mtwara Julai 12 na 13, 2019.

Lengo la kongamano hilo ni kuongeza ushindani katika soko, ushawishi wa kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa zao hilo ili kuongeza ajira na mapato. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 12, 2019 jijini Dar es Salaam  mkurugenzi wa kituo hicho, Godfrey Mwambe amesema hatua hiyo inatokana na kupoteza ajira na mapato mengi nchini kupitia usafirishaji wa korosho nje ya nchi.

“Kuna kitu kinaitwa mabibo, mabibo 15 katika korosho yana thamani kubwa kuliko korosho yenyewe, lakini pia kuna ganda la juu linatengeneza mafuta pamoja na kokwa la ndani linatumika katika mchanganyiko wa vyakula vya kuku,  hizi zote ni ajira katika mnyororo wa thamani.”

“Baada ya kuangalia kwa upana tangu mwaka 2018, TIC tulianza kufikiria namna ya kuzuia korosho zetu zisiende nje, ukipeleka malighafi utakuwa unapeleka ajira nje, wakati huo unaongeza umaskini kwa watu wako. Kongamano hilo ni fursa itakayokuwa na mrejesho wa umuhimu na matokeo ya uongezaji thamani,” amesema Mwambe.

Amebbainisha kuwa changamoto ya masoko katika zao hilo inahitaji kuwa na mwendelezo katika ufumbuzi wake.