In Summary

Mbali na kukamata bidhaa hizo, pia mamlaka hiyo imetaifisha bidhaa hizo pamoja na magari mawili 

Arusha. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata  mifuko 169 ya sukari yenye uzito wa kilo 50 kila mmoja pamoja na boksi 40 ya mafuta ya kupikia yaliyofungwa katika ujazo tofauti, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh20milioni.

Bidhaa hizo zilipaswa kulipiwa kodi ya Sh28.5milioni lakini kutokana na kuingizwa kinyemela, adhabu imeongezeka kwa Sh10.7 milioni, hivyo waliokamatwa sasa watapaswa kulipa Sh39.2milioni ya kodi na faini.

Mbali na kukamata bidhaa hizo, pia mamlaka hiyo imetaifisha bidhaa hizo pamoja na magari mawili yaliyotumika kupakia bidhaa hizo.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 16, 2018  na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere katika mkutano wake na waandishi wa habari na kubainisha kuwa Mei 11, 2018 eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani hapa,  mamlaka hiyo ilikamata malori mawili yakiwa yamepakia bidhaa za magendo.

Amesema  katika ukaguzi wa magari hayo walibaini yalikuwa yamebeba bidhaa tofauti, lori ya kwanza lilikuwa limepakia sukari.

Alisema kwamba lori jingine lilikuwa limepakia bidhaa mbalimbali ambazo ni mifuko 169 ya sukari na maboksi 40 ya mafuta ya kupikia aina ya Karibu yaliyofungwa kwa ujazo tofauti.