In Summary

Akizungumzia sababu za kutoonana na mtoto wake alisema walikosana baada ya kuacha shule lakini baadaye walielewana na kuendelea kuwasiliana kama kawaida.

Gerald Waya, baba wa msanii Agnes ‘Masogange’ amesema ameamua kumzika mwanaye pembezoni mwa nyumba yake ili asikae mbali naye tena.

Masogange aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge alikokuwa amelazwa kwa siku nne, anazikwa leo katika Kijiji cha Utengule wilayani Mbeya na mwili wake uliagwa jana katika Viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam. Akizungumza kijijini jana hapo, Waya alisema, “Nimetaka azikwe hapa karibu na nyumbani kwangu, nimewaomba kibali ndugu zangu cha kumzika Aggy hapa wamekubali, nimekaa mbali na binti yangu, sitaki tena hilo litokee mpaka nami nitakapoitwa mbele za haki.”

Waya alisema kwa mara ya kwanza ndani kipindi cha miaka 12 ataiona sura ya binti yake, lakini kwa bahati mbaya itakuwa ndani ya jeneza.

“Sijamuona Aggy muda mrefu, Jumapili iliyopita, Aprili 15 alipanga kuja kuniona baada ya kesi yake kuisha, bahati mbaya alianza kuumwa,” alisema.

Akizungumzia sababu za kutoonana na mtoto wake alisema walikosana baada ya kuacha shule lakini baadaye walielewana na kuendelea kuwasiliana kama kawaida.

Alisema Agnes ambaye ni mtoto wake wa nne kati ya sita, walikosana baada ya kumaliza elimu ya msingi katika Shule ya Utengule, Mbalizi alijiunga na Sekondari ya Sangu lakini aliacha akiwa kidato cha pili, “Alipata matatizo akiwa Sangu Sekondari, tukakosana akaondoka kwangu. Baadaye kama baba nilimsamehe mwanangu tukaendelea na mawasiliano kama kawaida.

“Aggy alikuwa msaada kwangu, hata nyumba hii alinijengea na amekuwa karibu na mimi. Kabla ya kufikwa na mauti alinipigia kuniaga. Aliniambia baba baibai.”

Alisema Masogange alimpigia simu, “Tukaongea naye akaniambia ‘mimi baba ninaumwa’. Nikamuuliza nini tatizo akasema, ‘aah! Baba niombee tu kwa Mungu’. Na Jumamosi iliyopita nilimpigia simu wakati yupo hospitali kujua maendeleo yake lakini akaniambia ‘baba bye’. Nikaanza kulia na hapo sikuwasiliana naye tena hadi nilipopata taarifa za kifo chake.”

Alisema mara zote alikuwa bega kwa bega na binti yake hasa kipindi cha matatizo aliyowahi kupitia.

Mwaka 2013, Masogange alikamatwa nchini Afrika Kusini akiwa na shehena ya kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya na mwaka jana alifikishwa mahakamani kwa makosa ya kutumia dawa za kulevya na Aprili 3 alitiwa hatiani na kutozwa faini ya Sh1.5 milioni.

Waya alisema katika kipindi chote cha matatizo ya mwanaye alikuwa akiwasiliana naye akimsihi kumrudia Mungu kwa kuwa ndiye anayeweza kumwokoa na majaribu yote.

“Wakati wa kesi alinipigia akaniambia baba nimeamua kuokoka, sitaki tena maisha ya kidunia nimemrudia Mungu,” alisema Waya.

Awakutanisha Ali Kiba, Diamond

Katika ibada ya kumuaga iliyofanyika kwenye Viwanja vya Leaders jana, wasanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Ali Kiba walikutana na kusalimiana.

Baada ya wasanii hao kusalimiana kwa kupeana mikono wakiwa meza kuu, baadhi ya waombolezaji walipiga kelele kushangilia. Diamond ndiye aliyeanza kumpa mkono Ali Kiba ambaye aliupokea kwa mikono yake miwili.

Baada ya tukio hilo, mshereheshaji wa shughuli hiyo, Emmanuel Mathias, maarufu MC Pilipili alisema: “Unaona sasa, hawana ugomvi hawa.”

Diamond na Ali Kiba wana ushindani mkubwa katika fani ya muziki, hivyo mashabiki wao kutengeneza makundi katika mitandao ya kijamii ya ‘Team Kiba na Team Diamond.’

Akitoa salamu zake, Ali Kiba ambaye ameoa mwishoni mwa wiki, alisema licha ya kwamba jana ilikuwa siku ya harusi ya mdogo wake Abdul Kiba, aliiacha na kwenda msibani kwa sababu vyote ni ibada.

Mwanamuziki Elias Barnabas (Barnaba) alilia na kushindwa kuendelea kuimba wimbo wa mwanamuziki Ambwene Mwasongwe, ‘Upendo wa Kweli’ wakati wa kuaga mwili wa Masogange.

Masogange alishiriki katika video ya Barnaba ya ‘Magubegube’.

Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) alighani shairi ambalo maneno yake yaliwaliza waombolezaji wengi.

Ibada ya kuaga mwili iliendeshwa na kiongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato la Makongo, Jeremiah, aliyesema kifo hakizoeleki na wala hakichagui wewe ni nani.