In Summary

Dk Mwigulu Nchemba amesema si sawa kumchukulia hatua mtu kwa kosa la mtu mwingine

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amesema si sawa kumchukulia hatua mtu kwa kosa la mtu mwingine.

Amesema hayo ikiwa ni siku 14 tangu Polisi wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kumkamata mama mjamzito Amina Mbunda na kumweka mahabusu kwa kosa la mumewe, Abdallah Mrisho.

Amina alikamatwa na polisi Mei 31 kwa kosa la mumewe aliyedaiwa kununua kitanda cha wizi. Aliwekwa mahabusu akiwa mjamzito na usiku wa kuamkia Juni Mosi, alishikwa uchungu na kujifungulia kando ya Kituo cha Polisi cha Mang’ula baada ya kukosa msaada wa kupelekwa zahanati.

Kutokana na tukio hilo lililoibua mjadala Juni 11, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiagiza Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kufuatilia suala hilo na kulieleza Bunge ilichobaini.

Spika Ndugai alichukua uamuzi huo baada ya mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali kuomba mwongozo wa Spika akidai kwamba kumekuwa na njama za kutaka kuficha ukweli kuhusu tukio hilo.

Jana, bungeni jijini Dodoma, Waziri Mwigulu wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devotha Minja aliyehoji tabia ya askari wa polisi wanapokwenda kumkata mtu wakimkosa wanamkamata mbadala, mke au mume alitaka kujua; “Jeshi la polisi wanatoa wapi mamlaka haya kwa kumkamata mtu na kumtesa?”

Waziri Mwigulu akijibu swali hilo alisema, “Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya kazi kwa mbadala, nielekeze kosa linabaki kwa mhusika na kama kuna mtu anaweza kusaidia afanye hivyo lakini si kuchukua adhabu kwa mtu mwingine.”

Hoja nyingine

Katika swali jingine la nyongeza mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliuliza, “Mwaka jana Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) alipotembelea Jimbo la Mtama aliahidi tukimaliza ujenzi wa kituo atatupatia gari, ni lini sasa tutapatiwa?” Akijibu, Dk Nchemba alisema ahadi hiyo itatekelezwa.

Katika swali na msingi, mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza aliuliza ni lini ujenzi wa ofisi ya wilaya ya kipolisi ya Mbalizi pamoja na nyumba za askari zitajengwa.

Njeza alitaka kujua Wilaya ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Waziri Mwigulu akijibu maswali hayo alisema Mbalizi ni miongoni mwa wilaya mpya za kipolisi zilizoanzishwa hivi karibuni. Alisema Jeshi la Polisi kwa kutambua ukosefu wa ofisi ya mkuu wa polisi wa wilaya pamoja na nyumba za makazi ya askari, linashirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kujenga ofisi ya mkuu wa polisi wilaya ambayo inajumuisha kituo cha polisi.

Waziri Mwigulu alisema ujenzi wa jengo hilo umefikia hatua ya umaliziaji, “Changamoto iliyobaki ni ujenzi wa nyumba za kuishi askari.”

Kuhusu idadi ya magari alisema wilayani hapo yapo matatu lakini moja ni chakavu linalohitaji matengenezo ili liweze kufanya kazi.

Alisema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Mbeya na kwingineko nchini kwa awamu kwa kutegemea rasilimali zilizopo na upatikanaji wa fedha.