In Summary

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella ametangaza utaratibu mpya wa mgawo wa mapato utakaotumika kwa wakulima wadogo wa mkonge na kampuni ya mkonge ya Katani Ltd iliyoasisi mpango wa kilimo cha mkonge kwa wakulima wadogo mkoani Tanga

Korogwe:  Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella ametangaza utaratibu mpya wa mgawo wa mapato utakaotumika kwa wakulima wadogo wa mkonge na kampuni ya mkonge ya Katani Ltd iliyoasisi mpango wa kilimo cha mkonge kwa wakulima wadogo mkoani Tanga.

Utaratibu huo ameutangaza leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wakati akizungumza na wakulima na viongozi wa Kampuni ya Katani Ltd alipotembelea mashamba matano ya mkonge yaliyopo wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Mbali na kutangaza utaratibu huo pia amesema madai kati ya wakulima wa mashamba matano ya mkonge  na kampuni hiyo umefikishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya kuhakiki madeni kati ya wakulima na kampuni.

Wakati CAG akilifanyia kazi jambo hilo, mtaalamu muelekezi ametoa taarifa kuwa katika mgawanyo kampuni hiyo itakuwa ikichukua asilimia 54 na wakulima asilimia 46.

Akiwa katika mashamba ya Hale, Ngombezi, Mwelya, Magunga na Magoma, Shigella amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kutokea hali ya sintofahamu kati ya kampuni hiyo na wakulima juu ya madeni halisi.

Amesema wakulima wanasema wanaidai kampuni hiyo fedha za mauzo ya mkonge kwa muda wa miezi tisa,  kuanzia Januari hadi  Septemba 2018 na wengine kuanzia Novemba 2017 lakini kampuni nayo inasema inawadai wakulima.

Amesema kufuatia mvutano huo wameona ni vyema jambo hilo kuchunguzwa na CAG ili kuhakiki madeni hayo na kujua uhalisia wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Katani Ltd, Juma Shamte amesema kampuni hiyo inawadai wakulima Sh3.8bilioni kuanzia 2006.