In Summary
  • Mbunge wa Gairo (CCM) Ahmed Shabiby amesema kuna mihemko katika upangaji wa mipango na kwamba bora kanda ya kati wangeletewa miche ya alizeti kwa sababu korosho mwisho wake itageuka kuni

Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM) Ahmed Shabiby amesema ni vema Serikali ingeleta mbegu za alizeti katika maeneo ya kati zitafanya vizuri kuliko miche ya korosho ambayo mwishowe itageuka kuni.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 9, 2018 wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2019/20.

Amesema kuna mihemko katika mipango na kwamba mwaka jana korosho ilivyopanda bei mikoa ya Kusini, Serikali imepeleka zao hilo katika mikoa mingine.

“Kwa kupanda bei kwa msimu mmoja tumeletewa kote. Nilikuwa naomba katika mipango yetu Serikali tuangalie twende kwa kanda,” amesema

“Tunajua kabisa ile miche iliyoletwa kwenye kanda yetu ya kati pamoja na Morogoro kama mngetuletea mbegu za alizeti tungefanya vizuri zaidi kwa sababu ndio maeneo yetu kwa sababu mnatuletea miche ya korosho mwisho itakuwa kuni tu.”

Amesema Serikali kufanya uchunguzi kuhusu suala la korosho kujua kama zipo kwa wakulima ama walanguzi ili kujua nani anataka kunufaika kwa zao hilo.

Mwisho