In Summary
  • Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Ijumaa Agosti 10, 2018

Ruangwa. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga Sh5bilioni katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa yenye urefu wa kilomita 57 kwa kiwango cha lami.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 10, 2019 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Likunja wilayani Ruangwa akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi wilayani hapa.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za jamii nchini kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ya Nanganga-Ruangwa-Nachingwea hadi Masasi unatarajiwa kuanza hivi karibu, amewataka wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Akizungumza kuhusu nyumba zilizowekewa alama ya X, Waziri Mkuu amewataka wahusika wazibomoe wenyewe ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kuwa walivamia eneo na watakaosubiri hadi Serikali iwabomelee watalazimika kuilipia gharama, hivyo ni vema wakatii.

Wakati huohuo, Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini, kwamba asilimia 95 ya vijiji vyote vya wilaya ya Ruangwa vinapata huduma hiyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya wananchi wa kata hiyo kueleza changamoto zinazowakabili ikiwemo huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

“Tumeendelea kuboresha huduma za jamii katika vijiji vyote vikiwemo na vya wilaya hii. Mkakati wetu ni kuhakikisha wananchi wote mnapata maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yenu na tayari asilimia 95 ya vijiji vinapata maji,” amesema.

Kuhusu changamoto ya zahanati ya kijiji cha Likunja kutokuwa na nyumba ya mganga, Waziri Mkuu amewashauri wananchi hao wafyatue matofali na kisha waanze ujenzi wa boma na halmashauri itawasaidia kuwapa vifaa vya viwandani kama saruji, mabati na misumari.