In Summary

Viwanda vyote vya sukari vyatakiwa kuwasilisha mapendekezo mapya juu ya mfumo mpya wa kusambaza bidhaa hiyo nchini ili kumpatia nafuu mlaji

Dodoma. Serikali imesema usambazaji wa sukari ili kusaidia bei kushuka hauwezi kuleta matokeo chanya kwasababu bei ya bidhaa hiyo hutegemea gharama za uzalishaji, usafirishaji na kodi ambavyo si rahisi kuviepuka.

 

Ufafanuzi huo ulitolewa leo bungeni mjini Dodoma  na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati akiwasilisha  kauli ya mawaziri kuhusu hali ya sukari nchini.

 

Alisema Serikali imefanya tathimini ya tasnia ya sukari nchini kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Machi hadi Agosti.

 

Hivi karibuni Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje aliihoji Serikali bungeni kwanini wananchi waendelee kusumbuka kutokana na bei ya sukari kuwa juu wakati bidhaa hiyo imejaa katika maghala viwandani.

 

Lubeleje alisema  bei ya sukari ipo juu ambapo inauzwa kati ya Sh2,600 hadi Sh3,000 kwa kilo lakini cha kushangaza imejaa katika maghala ya viwanda.

 

Akijibu hoja hiyo , Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya aliahidi kuleta mrejesho bungeni baada ya kukamilisha kulifanyia kazi suala hilo.

 

Leo, Waziri Mwijage aliwasilisha mrejesho huo na kubainisha kuwa, tathmini inaonyesha bidhaa hiyo inapatikana bila matatizo yoyote katika maeneo yote nchini.

 

“Takwimu za bei hadi kufikia Septemba 5 zinaonyesha wastani wa bei ya viwandani ni kati ya Sh1,746 na Sh2,160 kwa kilo. Kwa upande wa mauzo ya rejareja Mei ndio ilikuwa na bei ya juu ambapo kilo moja iliuzwa Sh2,900 mkoani Kigoma,” alisema.

 

Alisema bei ya chini ilikuwa ni Agosti   ambapo kilo moja ya sukari iliuzwa Sh2,300 kwa rejareja mkoani Morogoro na kwamba muhimu kuzingatia ni kuwa bei ya bidhaa hiyo ilianza kupungua taratibu baada ya msimu wa uzalishaji kuanza Mei.

 

Mwijage alisema tathmini inaonyesha kuwa katika kipindi cha kati ya Machi na Septemba hakukuwa na ongezeko kubwa la bei ya sukari nchini.

 

“Napenda kulihakikishia Bunge kuwa hakukuwepo upandaji wa bei mkubwa sana ila mabadiliko ya kati ya Sh50 mpaka Sh150 kutegemea mkoa na mkoa,” alisema.

 

“Kwa wastani wa bei za rejareja nchini ya juu ilikuwa kati ya Sh2,669 kwa Mei na bei ya wastani ya chini ikiwa Sh2,594 kwa Agosti.

 

Alisema tathimini ya sukari kimkoa inaonyesha mapungufu ya usambazaji ambapo mikoa ya Kigoma, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Mtwara na Njombe hununua sukari kipindi chote cha mwaka kwa bei ya juu sana kuliko mikoa mingine.

 

Mwijage alisema utafiti uliofanywa na Kampuni ya LMC International ya Uingereza mwaka 2014 kuhusu gharama za kuzalisha tani moja ya sukari nchini ulibaini inagharimu wastani wa Dola za Marekani 705.

 

Alisema kwa kutumia kiwango cha sasa cha kubadilisha Dola kwa Shilingi ni sawa na Sh1607 kwa kilo moja ya sukari na kwamba bei ya bidhaa hiyo inategemea kuimarika kwa Dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania.

 

Alieleza kuwa, viwanda vya sukari vinatumia mafuta, mitambo na vipuri ambavyo ni miongoni mwa bidhaa zinazopanda pindi Dola ya Marekani inapoimarika dhidi ya Shilingi ya Tanzania.

 

“Hii ni moja ya sababu inayochangia bei ya sukari kuwa kubwa au kubadilika mara kwa mara. Sababu nyingine ni mashamba mengi ya miwa kulimwa kwa kutumia mtindo wa kizamani ambao hauna tija kubwa,” alisema.

 

Alisema kufuatia tathimini hiyo, Serikali imetoa maelekezo kwa viwanda vyote kuwasilisha mapendekezo mapya juu ya mfumo wa kusambaza sukari nchini kwani  kuondoa udhaifu katika mfumo wa usambazaji wa bidhaa hiyo kunaweza kumpatia mlaji nafuu kidogo ya bei.

 

Kuhusu kurundikana kwa sukari katika maghala ya viwanda, Mwijage alisema suluhisho la tatizo hilo ambalo ni tishio kwa maendeleo ya viwanda vya sukari nchini ni kubuni utaratibu mpya wa kusimamia uagizaji wa kiasi cha upungufu wa sukari, kazi itakayokamilika kabla ya Oktoba mwishoni.

 

Kwa upande wa gharama za uzalishaji, alisema Serikali inafuatilia mpango wa viwanda kuongeza tija katika mashamba ya miwa hali itakayopelekea gharama za uzalishaji kushuka.